ELIZABETH CHEPKORIR: Aliwakeketa wasichana 1,000 lakini sasa anaongoza kampeni za kukomesha uovu huo
Na MAGDALENE WANJA
KATIKA miezi ya Novemba na Desemba, baadhi wanawake na wasichana katika kaunti za Nakuru na Baringo hutarajiwa kukeketwa.
Hii ni licha ya tamaduni hizo kupigwa marufuku kutokana na hatari inayotokana na kukeketwa kama maradhi ya pepopunda na hali ya unyanyapaa.
Licha ya hayo, baadhi ya waliokuwa wakitekeleza tamaduni hizo wamebadili mienendo yao na kwa sasa wanajihusisha katika kampeni za kupigana na utamaduni huo.
Kwa zaidi ya miaka 10, Bi Elizabeth Chepkorir alijihusisha na ukeketaji wa wanawake na wateja wake walikuwa kutoka kaunti za Nakuru na Baringo.
Bi Chepkorir ambaye sasa ana umri wa miaka 66 anasema kuwa kwa muda mrefu ambao alitekeleza ukeketaji, zaidi ya wanawake 1,000 walipitia mikononi mwake.
“Nilijifunza ukeketaji kutoka kwa nyanya yangu ambaye alikuwa amefanya tamaduni hii kwa muda mrefu. Ilinichukua mwaka mmoja peke yake kujifuinza ujuzi wote na ndipo nikaanza kazi hiyo,” akasema Bi Chepkorir.
Bi Chepkorir alisema kuwa ijapokuwa hakuwa na ujuzi wowote kuhusu uzazi, familia za waliokeketwa walimuachia wasichana wao kuwakeketa bila kujali.
“Nyanya yangu alitaka niridhi ujuzi huo kutoka kwake na kwa hivyo ilinilazimu kutia bidi zaidi,” anasema.
Biashara ilinoga
Akisimulia jinsi alivyotekeleza kitendo hicho, Bi Chepkorir alisema kuwa biashara hiyo ilinoga sana wakati wa likizo za shule.
Baadhi ya wateja wake walikuwa wanawake ambao walikuwa tayari wameolewa na waliletwa na waume zao ambao walidai kuwa hawawezi kustahimili mwanamke ambaye hajakeketwa.
“Shughuli ya ukeketaji ilifanyika kichakani karibu na nyumbani kwangu kwani nilihofia kukamatwa,” akasema.
Aliifanya shughuli hiyo wakti wa usiku wa giza totoro wakati wakazi walikuwa usingizini.
Kinyume na wakeketaji wengi ambao huogopa kusimulia visa walivyovishudia wakati wa ukeketaji, Bi Chepkorir ana ujasiri wa kutoa hadithi zake.
“Sikuwa na vifaa maalum vya kukeketea kwani wakati mwingine nilitumia kisu ambacho kilinolewa siku moja kabla ya shughuli hiyo. Wakati mwingine nilitumia wembe,” aliongeza.
Kutokana na ukosefu wa ujuzi kuhusu afya, wakati mwingine wasichana waliopitia mikononi mwake walipatwa na maradhi mabaya.
Waliokeketwa hawakutumia dawa zozote za kusaidia kuponya vidonda kwani kutembelea hospitali kungepelekea kukamatwa.
Ada ya Sh200
“Kila aliyekeketwa alilipa Sh 200 na kiwango hiki cha pesa kilinipa raha sana japokuwa tulipigana mara kwa mara na mume wangu kwani hakupendelea ukeketaji,” anasimulia.
Kiwango cha pesa alizopata alizitumia kununa vileo ambavyo alitumia kupunguza mawazo na kumpa ujasiri alipokuwa aikeketa.
Kiasi kilichobakia, alikitumia kulisha jamii yake.
Biashara yake ilinoga na aliwavutia wateja wengi hadi siku moja alipoletewa mwanamke mjamzito kumkeketa.
Mwanamke huyo aliyekuwa na uja uzito wa miezi minne alikwa mwenye umri wa miaka 15 na aliletwa na mumewe.
“Hakuwa mwanamke wa kwanza mjamzito ambaye nilitahiri na hivyo niliendelea na shughuli hiyo kwani lilikuwa ni jambo la kawaida,” akasema Bi Chepkorir.
Baada ya kukeketwa, mwanamke huyo alifuja damu sana na juhudi zote alizofanya kumwokoa hazikufua dafu.
Mafichoni
Aliamua kutoroka huku akimuacha mwanamke huyo katika hali mahututi kwani alihofia kukamatwa.
Wakazi wa kijiji hicho walimsaidia na kumpeleka hospitalini huku Bi Chepkorir akijificha msituni.
“Chifu wa eneo hilo alikuja kunitafuta na kunishauri nirudi nyumbani kwani mwanamke huyo alikuwa ashapona tayari,” alisimulia.
Kutokana na tukio hilo, Bi Chepkorir aliamua kuiacha kazi ile kwani aliona kuwa ilikuwa inahatarisha maisha.
Bi Chepkorir sasa ni balozi wa kupigana na ukeketaji wa wanawake. Hata hivyo, tamaduni hiyo imasalia kuwa changamoto katika maeneo ya Baringo na Nakuru.
Katika kaunti ya Nakuru maeneo yaliyoathirika zaidi ni Njoro, Molo and Rongai.
Bi Sally Wuod, ambaye ni afisa wa jinsia katika shirika la Dandelion Africa linalopigana na ukeketaji, alisema kuwa watekelezaji wa tamaduni hiyo hufanya kwa usiri wa hali ya juu.
“Wakati wakeketaji hao wanapogundua kwamba wanafuatwa, huwa wanahamia katika vijiji vingine ambapo wanatekeleza shughuli hiyo,” akasema Bi Wuod.
Shirika hilo limekuwa likiendeleza kampeni ya kupigana na ukeketaji kwa kuwahusisha wanaume na wanawake katika uhamasisho.