Wakulima Nyeri kupata soko la mazao nchini Amerika
LUCAS BARASA Na SOPHIA WANJIRU
SERIKALI ya Kaunti ya Nyeri imeingia kwenye ushirikiano wa kibiashara na Amerika kusaka soko kwa mazao yanayotokana na kilimo.
Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga alisema Ijumaa kuwa ushirikiano huo utawanufaisha wakulima ambao wamekuwa wakiteseka kupata masoko kwa mazao na bidhaa zao.
“Nyeri ni kati ya maeneo ambayo yanategemewa na nchi katika kuzalisha chakula. Ni vyema kuwa kupitia ushirikiano huu, wakulima wetu wa kahawa avokado na majanichai watapata soko kwa mazao yao,” akasema Bw Kahiga.
Alikuwa akiongea afisini mwake ambako alikuwa ametembelewa na Balozi wa Amerika nchini Kenya, Meg Whitman.
Bw Kahiga aliwataka wakulima wa kahawa wakumbatie upanzi wa mbegu ambazo zinanawiri vizuri ili kuongeza uzalishaji. Alisifu Amerika kwa kuchangia kuimarika kwa sekta ya afya katika kaunti hiyo kupitia kuanzishwa kwa maabara na kuleta vifaa vya kimatibabu.
Whitman alisema kuwa Amerika itaendelea kushirikiana na kaunti hiyo hasa katika sekta ya uvumbuzi wa teknolojia. Wakati wa ziara yake Nyeri, balozi huyo alitembelea Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Dedan Kimathi ambako kituo cha kisasa cha sayansi kinajengwa.
Bw Kahiga na Bi Whitman pia walijadiliana kuhusu kuimarisha utalii ikizingatiwa kuwa Nyeri ina maeneo mengi ya kitaliil. Kati ya maeneo hayo ni Mlima Kenya na Mlima Aberdare.