NMG yapeleka msaada kwa kituo cha watoto cha Mama Fatuma
NA SAMMY KIMATU
WATOTO katika makao ya Mama Fatuma Goodwill Children’s Home katika mtaa wa Eastleigh Section 1, kaunti ndogo ya Kamukunji wana kila sababu ya kutabasamu baada ya Wakfu wa Nation Media (NMF) kuwapiga jeki kielimu na kiafya.
Wakiongozwa na Meneja wa Wakfu wa Nation Media (NMF) Daisy Maritim Maina, wafanyakazi wa kampuni ya Nation Media Group (NMG) walizuru makao hayo ya watoto siku ya Ijumaa ili kuwapatia msaada kama zawadi wakati huu wa likizo ya muhula wa kwanza.
Bi Maina, akishiriana na Mshirikishi wa Kitengo cha Uhusiano Mwema katika NMG Naomy Ikenye, waliongoza wafanyakazi katika harakati za kutangamana na watoto hao kabla ya kilele cha hafla yenyewe kufika.
Watoto walitumbuiza wageni wao kwa nyimbo huku nyuso zao zikionyesha tabasamu.
Bi Maina alisema kwamba nia ya kuyatembelea makao hayo ilikuwa ni kuwajali wengine katika jamii hasa msimu huu wa Mfungo wa Ramadhani kwa Waislamu sawia na sherehe za Pasaka kwa walio Wakristo.
“Lengo la NMF ni kufikia na kushirikisha jamii ili jamii ijihisi iko pamoja na wengine. Pia kampuni ya NMG imeshirikiana na MFCH kwa zaidi ya miaka 10 ambayo imepita,” Bi Maina akasema.
Vilevile, katika hotuba yake, meneja wa Makao ya Watoto ya Mama Fatuma, Bw Mohammed Hiribae alishukuru NMF kwa msaada waliotoa akisema bidhaa walizopokea bila shaka ni kwa manufaa ya elimu na malezi ya watoto wanaoishi katika makao yale.
Aliongeza kwamba kuna ongezeko la dhuluma kwa watoto akisema kwamba nyingi zake zikichangiwa na mizozo ya walio katika ndoa na pia wasichana kutelekezwa waume watarajiwa.
Zaidi ya hayo, Bw Hiribae alisema kwamba mambo hayo huchangiwa na ukosefu wa ukumbatiaj wa maadili mema na matumizi ya mihadarati.
Kadhalika, Wakfu wa NMF ulisambazia watoto msaada wa chakula mseto ikiwemo unga wa ugali, unga wa ngano, mchele na sukari.
Isitoshe, pia walipeana mafuta ya kujipaka, sabuni, sodo za wasichana waliobaleghe, rangi ya kupaka viatu, maji, soda na vitafunio miongoni mwa bidhaa nyingine