Gavana aonya wanaotoza chekechea karo
NA WINNIE ATIENO
GAVANA wa Mombasa Abdulswamad Nassir ameonya bodi za shule za chekechea dhidi ya kuwatoza wazazi karo ya shule.
Hii ni baada ya serikali hiyo kuamua kutotoza wanafunzi hao wa chekechea karo ya shule.
Kwenye mkutano na baraza la mawaziri wa kaunti afisa mkuu Dkt Noah Akala alisema kaunti hiyo imeamua kuwalipia zaidi ya wanafunzi 7000 karo ya shule ya Sh3200.Hata hivyo kwa mujibu wa katiba, na Mswada wa Elimu ya Shule za Msingi, elimu ya shule ni bure.
Katika kaunti nyingi wanafunzi hawatozwi karo.
“Katika shule nyingi hapa Mombasa bodi za usimamizi zimekuwa zikiwatoza wanafunzi wa shule za chekechea karo. Lakini serikali ya kaunti imeamua kufadhili masomo hayo ili kupunguza gharama kwa wazazi,” alisema Dkt Akala.
Akiongea na Taifa Leo, Bw Akala alisema wazazi walikuwa wanashurutishwa kugharamia fedha za vitabu na bodi zinazosimamia shule hizo. Dkt Akala alisema serikali ya kaunti imemwamuru waziri wa Elimu kuhakikisha wazazi hawatozwi karo yoyote.
“Elimu ya chekechea imegatuliwa, kwa hivyo ni serikali za kaunti zinazosimamia shule hizo kwa mujibu wa Katiba,” aliongeza.
Alisema kuanzia mwaka mpya wa kifedha, wakazi watanufaika na elimu ya bure ya chekechea. Vilevile wanafunzi hao wataendelea kupokea lishe bora (chakula cha mchana).
Kwenye mkutano huo, serikali hiyo pia ilipendekeza mageuzi kadhaa ili kuimarisha ugatuzi na kuimarisha maisha ya wakazi.
Ili kuimarisha sekta ya uchukuzi serikali ya kaunti imewasihi wakazi kutumia bodaboda, kutembea na uendeshaji wa baiskeli. Malori yanayosafirisha bidhaa hatari ikiwemo gesi au petroli zitatakiwa kusafiri kwa saa ili kuzuia ajali.
“Ili kuimarisha usalama barabarani hasa kwa wapita njia, serikali ya kaunti itaweka taa mitaani. Hatua hii pia itadumisha usalama mitaani na kurembesha jiji letu la kitalii,” aliongeza Dkt Akala.
Dkt Akala alisema Gavana Nassir pia ameweka mikakati kudhibiti ugubiaji wa vileo. Hii ni baada ya kutia saini Mswada wa Kusimamia Leseni za vileo 2024.
Kwenye mswada huo, serikali ya kaunti itajitwika jukumu la kutumia ushuru wa leseni za maeneo ya burudani, baa kurekebisha waraibu sugu wa mihadarati. Dkt Akala alisema mswada mpya wa kusimamia leseni itaimarisha sekta hiyo.