Wakulima na wafugaji 41,000 kugawana Sh393.6m za kaunti kwa kadi maalum
NA MWANGI MUIRURI
GAVANA wa Murang’a Irungu Kang’ata ataanza kuwapa wakulima na wafugaji wa eneo hilo Sh393.6 milioni kila mwaka kama fidia ya kupunguza gharama za uzalishaji na pia za wao kujipa raha kidogo.
Dkt Kang’ata alisema kwamba atakuwa akitoa kadi maalum iliyojazwa kwa Sh2,400 kwa kila mkulima ambaye atasajiliwa kwa mpango huo.
“Pesa hizo zitakuwa zikitolewa kila baada ya miezi mitatu na katika mwaka wa 2024, jumla ya wakulima 41,000 watanufaika,” akasema Dkt Kang’ata.
Kaunti ya Murang’a kwa mujibu wa Sensa ya 2019 iko na takriban wakulima 320,000 na ikiwa kila mwaka kutakuwa na lengo la kufaidi 20,000 kati yao, ina maana mpango huo utawafikia wote katika kipindi cha miaka 16.
Kizungumkuti ni kwamba, awamu ya mwisho ikifikiwa kunufaika, kuna wale watakuwa wamepata pesa hizo kwa miaka 15 huku wa mwisho wakipata kwa mwaka wa kwanza hivyo basi kuzua suala la haki na usawazishaji.
Gavana Kang’ata iwapo atapata awamu ya pili mamlakani, atakuwa afisini hadi 2032 huku mpango huo ukitazamiwa kuwakumbatia wakulima wote mwaka wa 2050.
Kiongozi huyo alizindua usajili wa wakulima mnamo Machi 18, 2024, katika shirika la maziwa la Kigoro katika eneobunge la Gatanga.
Alisema kwamba kadi hiyo inaweza ikatumika kununua bidhaa za ufugaji, kulipa karo na pia kugharimia huduma za kimatibabu.
Alisema kwamba iwapo mkulima hatakuwa ametumia pesa hizo katika kipindi cha miezi mitatu ambapo mjazo mwingine wa pesa utawekwa, hatakuwa akipoteza salio katika kadi.
“Hatutakuwa tukiondoa pesa zile ambazo hutakuwa umetumia katika mjazo wako. Ni wakati sasa wa wakulima na wafugaji matajiri watupe nafasi ya kusaidia wale wa kiwango cha chini,” akasema.
Katika awamu ya kwanza ya mpango huo ambayo Bw Kang’ata alizindua Aprili 2, 2023, wafugaji wa ng’ombe wa maziwa walikuwa wakipata Sh3.50 kwa kila lita ya maziwa yaliyowasilishwa katika vyama vya ushirika huku nao wakulima wa maembe wakipata Sh7 kwa kila kilo waliyowasilisha kwa kampuni za ununuzi. Kwa ujumla, kulikuwa na wakulima 21,000 ambao walikuwa wamesajiliwa na walikuwa wakipata pesa hizo kila mwezi.
Ni mpango ambao mkulima mmoja alikuwa akipata hata Sh170,000 lakini kwa sasa katika awamu mpya itakayoanza kutekelezwa Aprili 1, 2024, kila mkulima atakuwa akipata Sh2,400.
Swali lingine ambalo limechipuka ni kuhusu wakulima walio nje ya uzalishaji wa maziwa na maembe ambao kwa sasa baadhi yao ndio wanatuzwa pesa hizo za kaunti ikizingatiwa kwamba kaunti ya Murang’a iko na zaidi ya aina 150 za kilimo.
Hao wa maembe na maziwa ambao wanalengwa Bw Kang’ata amesema wanajumuisha asilimia 73 ya wote walio katika Kaunti.