Joshua Waiganjo: Mfungwa aliyerushwa ‘Jehanamu’ apata ukombozi mpya akilenga fidia ya Sh1.5B
WANDERI KAMAU Na JOSEPH OPENDA
LICHA ya kuondolewa mashtaka yaliyokuwa yakimkabili na mahakama mnamo Alhamisi, Joshua Karianjahi Waiganjo anafanana na mtu aliyetupwa Jehanamu yenye moto mkali na hatimaye kufufuka.
Mnamo Alhamisi, Waiganjo alipata afueni baada ya kuondolewa shtaka la kujifanya maafisa wa ngazi za juu za polisi katika eneo la Bonde la Ufa na mahakama ya Naivasha.
Waiganjo aligonga vichwa vya habari miaka 11 iliyopita, baada ya mashtaka yake kuitikisa nchi nzima.
Baadhi ya makosa ambayo Bw Waiganjo alikuwa akikabiliwa nayo ni mashtaka manne ya kujifanya maafisa wa ngazi za juu wa polisi, kumiliki sare za polisi kinyume cha sheria na mashtaka mawili ya wizi wa kimabavu.
Akitoa uamuzi wake, Hakimu Mkuu wa Naivasha, Bw Nathan Lutta, alirejelea uamuzi uliotolewa mnamo 2017 na Mahakama ya Rufaa, ulioagiza mshtakiwa huyo kuachiliwa huru.
Hakimu aliongeza kuwa uamuzi wa mahakama hiyo ulikuwa umemwondolea Waiganjo mashtaka ya visa viwili vya wiizi wa kimabavu, baada ya walalamishi kukosa kutoa ushahidi wao mahakamani.
Hata hivyo, Waiganjo alihukumiwa kifungo cha miaka mitano gerezani kwa kujifanya polisi, mwaka mmoja kwa kuvalia sare za polisi na miezi sita kwa kosa la kuwa na vifaa vilivyokuwa vimetolewa katika maghala ya serikali.
Kuachiliwa kwake bila shaka kunafananishwa na makosa yaliyowakabili wahalifu sugu nchini katika miaka ya hapo nyuma kama John Matheri, Wanugu, Wacucu kati ya wengine wengi.
Kulingana na mfungwa wa zamani John Kibera, ambaye alikuwa mwizi sugu wa benki katika miaka ya 1970, makosa aliyofanya Waiganjo “si ya mtu wa kawaida”.
Anasema kuwa, ikiwa ni kweli Waiganjo alitangamana na maafisa wa polisi wa ngazi za juu na hata kuwa na sare za polisi, basi hilo linaonyesha kuwa kuna uwezekano kuna watu wenye ushawishi aliokuwa akishirikiana nao kwa karibu katika Idara ya Polisi.
“Ukweli ni kuwa, haya si makosa ambayo hufanyika vivi hivi tu. Lazima alipata usaidizi kutoka kwa watu wa ndani katika idara hiyo. Haya ni mambo niliyoshuhudia nikiwa gerezani katika miaka ya 1980,” akasema Bw Kibera kwenye mahojiano.
Hata hivyo, anasema kuwa kufutiliwa mbali kwa mashtaka ya Bw Waiganjo ni “ukurasa mpya ambao amepata katika maisha yake, hivyo jamii inafaa kumkubali bila kumhukumu”.
“Gerezani ni kama Jehanamu. Hakuna anayetamani kuwa gerezani. Hata hivyo, kuachiliwa kwake ni sawa na kufufuka upya kimaisha,” akasema.
Waiganjo mwenyewe
Aliachiliwa chini ya Ibara ya 210 ya utaratibu wa kesi za ulaghai, ambapo aliondolewa mashtaka yote.
Sasa anasema kwamba analenga kuwasilisha kesi mahakamani alipwe fidia ya Sh1.5 bilioni. Baadhi ya mawakili wake Danstan Omari na Gordon Ogolla.
Anasema alitendewa hujuma, hali iliyofanya ataabike kihisia, kijamii na kifedha kwa miaka 11.
Mbali na kushtakiwa kujifanya maafisa wa polisi, pia alikabiliwa na tuhuma za mauaji ya polisi 40 na majangili katika Kaunti ya Samburu, mauaji yanayofahamika kama ‘Baragoi massacre’.
Mashtaka mengine yalikuwa ni wizi wa mabavu, kuwahangaisha wafanyabiashara na wizi wa lori.
Baada ya miaka kadhaa ya kujitetea, hatimaye uamuzi wa mahakama ya Naivasha ulimuondolea lawama.
Hakimu Mkuu Nathan Lutta ndiye aliyemwondolea lawama Bw Waiganjo.
Sasa Bw Waiganjo anasema hana budi kupambana na waliomwekelea mashtaka.
“Ukimpeleka mtu mahakamani bila ushahidi kisha aachiliwe, ni lazima uwe umejiandaa kulipia,” akasema Bw Waiganjo.
Anadai kesi hiyo ilimchafulia jina na kusababisha yeye kupoteza marafiki.
“Aidha, babangu aliaga dunia kwa sababu kesi dhidi yangu ilimuathiri sana,” akasema.
Anaongeza kwamba aligeuzwa mume gumegume ambaye alishindwa kuichumia familia yake.