Makala

Wizi wa punda waongeza mahangaiko ya maji, kulemaza biashara Moyale

March 30th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA FRIDAH OKACHI

WAMILIKI wa punda, eneo la Heilu, Kaunti ndogo ya Moyale, Kaunti ya Marsabit wanalalamikia idadi ya punda wao kupungua kutokana na wizi.

Upungufu huo wa punda umechangia jamii hiyo kuathirika ambapo sasa wafanyabiashara wanahangaika wakitaka kupeleka bidhaa zao sokoni.

Aidha, wakazi wanaotegemea wanyama hao kubeba maji kutoka kwenye bwawa la Heilu wamelazimika kubeba vibuyu kichwani na kutembea mwendo mrefu wakiwa wamebeba maji mazito.

Punda wawili wakiwa njiani kuelekea nyumbani na maji. PICHA | FRIDAH OKACHI

Mkazi Fatuma Dalle, mama wa watoto sita, anayemiliki punda wawili wanaomsaidia kutekeleza majukumu ya nyumbani, aliambia Taifa Leo kwamba yeye hufika kwenye bwawa hilo majira ya asubuhi kuteka maji. Kisha yeye huyabeba akisaidiwa na punda wake wanaosambaza kwa wateja wake katika mji wa Moyale.

“Punda hawa hunisaidia kuja kwenye bwawa hili majira ya asubuhi na jioni. Na mimi huja nao hapa safari nane kila siku. Mchana huwa ni wakati wangu kuenda kutafuta kuni ambazo hubebwa na punda hao,” akasema Bi Dalle.

Bi Fatuma Dalle akizungumzia umuhimu wa punda. PICHA | FRIDAH OKACHI

Hofu yake ni kuwa wezi wanaweza wakaiba punda wake na kumuacha na kilio.

Anasema wezi wa wanyama hao wanarejesha shughuli zao nyuma.

“Kuna wale kutoka taifa jirani huomba punda na kuturudishia. Lakini punda wako akipotea anachukuliwa na mtu anayekujua,” anasema.

Mkazi Abdi Dida ambaye pia anamiliki punda, anasema wezi wakishaiba punda, huwasafirisha ama asubuhi au usiku. Anadai kuwa, kuna magari malori ambayo hutumika kutekeleza shughuli hiyo.

“Gari moja hubeba punda kama 40 kumaanisha kwa siku ni punda zaidi ya 80 wanaopotea,” anaeleza Bw Dida.

Kulingana Bw Dida, ununuaji wa punda kutoka kwenye eneo la mpaka wa Ethiopia na Moyale umechangia kupotea zaidi kwa wanyama hao.

“Punda wakionekana wametelekezwa mtaani wakirandaranda, huwa wanachukuliwa na wezi,” anasema.

Ili kuwatambua punda, wao huweka alama maalum.

Afisa wa Mifugo, Kaunti ndogo ya Moyale, Bw Hassan Nura Guyo, anaambia Taifa Leo kutatua suala hilo, Kenya inafaa kuangalia upya sheria ya kupiga marufuku vichinjio vya punda.

“Sheria yetu ina matatizo. Ilipiga marafuku ya uchinjaji wa punda kwenye vichinjio lakini ikaipa jamii fulani ruhusa ya kula nyama ya punda,” akasema Bw Guyo.

Afisa wa mifugo Kaunti ya Marsabit Bw Hassan Nura Guyo. PICHA | FRIDAH OKACHI

Afisa huyo pia analalamika kwamba wanaosafirisha wanyama hao, mara nyingi huwa wametafuta idhini kupitia mlango wa nyuma.

“Huo usafirishaji unafanya eneo hili kupoteza punda 70,000. Iwapo idadi hii itapungua zaidi, wanawake wanaowategemea kufanya kazi wataumia sana,” akasema Bw Guyo.

Meneja wa Programu katika Shirika la Ustawi wa Wanyama Afrika (Africa Network for Animal Welfare) Dennis Bahati, anasema uchinjaji wa punda kwenye vichaka umeongezeka.

“Pia kuna punda wanaoingizwa Kenya kutoka Ethiopia na wanapatana na wengine na kupelekwa kwenye vichijio. Wanapelekwa maeneo ya Ndeiya na Kapsoit ambapo baada ya kuchinjwa, nyama yao inauziwa umma bila kujua ambapo ni kinyume na Sheria,” anasema Dkt Bahati.