Habari za Kitaifa

Ndoa zasambaratika kwa vijana kutafuta ajira majuu – Askofu

March 30th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA SAMMY KIMATU

TATIZO la ukosefu wa ajira nchini limechangia vijana wengi nchini kuenda ughaibuni na kuacha ndoa zao changa zikiwa mashakani, amesema askofu mmoja jijini Nairobi.

Akiongea wakati wa ibada ya Pasaka sikukuu ya Ijumaa Njema, Askofu Mkuu wa Kanisa la Jesus Restoration Christian Church (JRCC), Dkt Joseph Njoroge, katika eneo la Njiru, kaunti ya Nairobi, Bw Njoroge alisema vijana wanasafiri ughaibuni na kuacha mwanya mkubwa katika mahusiano, hali inayochangia ndoa kusambaratika au mipango ya ndoa ya wachumba kufutika.

“Mwanamke akienda ng’ambo anamuacha mchumba wake katika hali ya upweke. Changamoto ni kwamba mume na mke au wachumba wakitengana kwa kati ya miaka miwili au mitatu, mahusiano kati ya wawili hao huingia doa,” Dkt Njoroge akasema.

Anaitaka serikali kuangazia kwa kina ongezeko la vijana kusafiri ughaibuni kusaka ajira huku wakiacha Kenya likiwa taifa la taabu.

Aidha, alisema kuongezeka kwa uhalifu kunachangiwa na utumiaji wa mihadarati miongoni mwa wanajamii na hivyo kuna umuhimu wa hatua za kudhibiti janga hilo.

Hii ndio sababu Dkt Njoroge aliunga mkono serikali katika vita vinavyoendelea vya kusaka pombe haramu, akisema inachangia pakubwa katika mizozo ya ndoa na kuzembea kwa vijana wanaoshindwa kufanya kazi kujenga taifa.

Kadhalika, Dkt Njoroge alisema kanisa ni nguzo kubwa katika nchi na kuongeza kwamba jukumu la asasi hiyo ni kuwakuza watu kiroho ili wawe na maadili mema.

Aidha alisema kanisa lina wajibu muhimu kuishauri serikali.

Aliitaka serikali kuweka zingatio katika kutatua changamoto iliyopo ya mgomo wa madaktari.

Pia alitoa himizo kwa serikali iwe ikitoa pesa za mgao wa shule mapema ili masomo yasiathirike.