Habari za Kaunti

Gavana Mwangaza ataja vitisho kiini cha kutotembelea Igembe

March 31st, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA DAVID MUCHUI

GAVANA wa Meru Kawira Mwangaza alifichua kuwa vitisho vya kila mara kutoka kwa wapizani wake ndio sababu kuu ya kukaa mbali na eneo la Igembe kwa miezi mitatu iliyopita.

Akihutubia wakazi wa eneo la Igembe walioandamana hadi afisini mwake kumtaka alitembelee, Gavana Mwangaza alisema aliepuka eneo hilo baada ya kushambuliwa na wahuni wakati wa ziara ya Rais William Ruto mnamo Januari, 2024.

“Mara ya kwanza nilishambuliwa mwaka jana (2023) baada ya kutoa msaada wa ng’ombe huko Maua. Niliepuka kundi la watu wenye ghasia kwa neema ya Mungu. Nilipoandamana na rais hadi Igembe, nilipigiwa kelele. Gari langu lilivamiwa na wahuni waliokuwa wakitafuta damu yangu,” alisema Gavana.

Alimshutumu Mbunge wa Igembe ya Kati Bw Dan Kiili na Waziri wa Kilimo Mithika Linturi kwa kulipa vijana ili kumkashifu mbele ya rais.

Hata hivyo, madai hayo yalikanushwa na Bw Kiili.

Bi Mwangaza alisema wapinzani wake wa kisiasa pia walijaribu kumhusisha na mauaji ya mwanablogu Daniel Muthiani, na kufanya eneo hilo kuwa na uadui naye.