Mama wa miaka 55 afichua siri kudumisha nywele za rasta
NA MWANGI MUIRURI
MAMA wa miaka 55 kutoka Kaunti ya Nairobi ambaye amefuga rasta kwa miaka 15 hadi sasa anasema nywele hizo huhitaji sanasana lishe ya ndizi, nduma na ngwaci ambazo zimekaangwa kisha kuteremshwa na miwa.
Bi Elizabeth Wangumburu anasema kwamba isiwe ni juisi ya miwa, bali iwe ni muwa uliovunwa mzimamzima uuchambue kwa meno yako mwenyewe.
“Wengi wa waliolea nywele aina ya rasta huishia kuwa wanyonge na wakonde kutokana na ukosefu wa lishe bora inayohitajika kutoa madini muhimu ya kuzilea zikiwa na afya na rangi nyeusi. Siri yangu ambayo ninakufichulia ni kwamba uwe ukizipa chakula asili kisha kama kawaida, ujizoeshe kuwa ukipata usingizi wa kutosha,” akasema.
Anasema kwamba aliafikia uamuzi wa kulea nywele hizo kutokana na imani yake kwamba huwa zinazua nembo ya watu walio wapole na wenye roho safi.
“Mimi niliamua kuzilea kama imani ya kushikilia upole na wema wa roho. Sikufanya hivyo ili kushindana na wengine lakini zikiafikia kigezo cha kumbukumbu za rekodi za dunia nitashukuru,” asema.
Bi Wangumburu alisema kuwa siku hizi hata huogopa akitembea na nywele hizo mitaani kutokana na vile wengi huzitamani.
“Hata huwa sipendi wengi wazigusaguse. Huwa zinazua uvutio mkuu kwa wengi. Hata nimekataa watu kunisaka wakitaka kuziona. Lakini nashukuru kwamba wengi huzichukulia kama nembo yangu ya kipekee,” asema.
Anasema kwamba nywele hizo hazihitaji utunzaji wa bei ya juu ili kudumisha usafi kama wengi wanavyodhania.
“Mimi mbinu yangu huwa ni rahisi ambapo zikioshwa tu, hupakwa mafuta spesheli na kunyunyiziwa maji kidogo halafu nazikausha kupitia jua. Hakuna mambo ya kuingia kwa mashine za saluni,” asema.
Alisema kwamba anaweza akawapa wote walio na nia ya kulea nywele mtindo huo mawaidha ya bure.
“Yangu sio biashara. Ni hali ya maisha ambayo nimejiamulia kwa hiari yangu na kwa raha zangu. Ninapata raha kuu kutembea na rasta zangu ambazo huwa nazifunga ili zisining’inie kwa mgongo. Nikiziachilia zitaenda zikifagia chini,” aringa.
Kwenye mahojiano na Taifa Dijitali, Bi Wangumburu alisema kwamba anapania kuzilea hadi mwisho wa uhai wake “na kwa wakati huo nitaamua ikiwa nitaziacha kwenye makavazi au nisonge nazo tu katika maisha mapya ya kuzimu”.