Utasukumwa jela kwa kukosa kumeza dawa kwa mujibu wa maelezo ya daktari
NA BENSON MATHEKA
UNAJUA kwamba unaweza kufungwa jela kwa kukosa kumeza dawa unavyoagizwa na daktari?
Unajua kukosa kuzitumia ipasavyo ni tishio kwa usalama wa taifa pale unapougua ugonjwa wa kuambukizwa?
Wakenya wengi hawazingatii sheria zinazowalinda binafsi na watu wanaotangamana nao.
“Ni haki ya mgonjwa kufuata ushauri wa daktari na kumeza dawa zote kama anavyoagizwa na daktari. Kwenda kinyume na maagizo ya daktari ni kuvunja sheria,”asema Dkt Robert Kiingati wa hospitali ya Aga Khanm Nairobi na kuongeza kuwa Wakenya wengi wamekuwa wakipuuza baadhi ya sheria rahisi lakini muhimu kwa maisha yao.
Mnamo 2012, mahakama ilisukuma jela Daniel Ngetich na Patrick Kipngetich waliougua ugonjwa wa kifua kikuu kwa kukataa kumeza tembe za kuwatibu.
Mahakama iliwapata ndugu hao na hatia ya kuwa tisho kwa umma.
Kulingana na sheria za afya ya umma ya jamii, kuzuia kuenea kwa maradhi ni muhimu kuliko maslahi ya mtu binafsi.
Wagonjwa wanaopatikana wakiugua maradhi ya kuambukizana wanaweza kuzuiwa kwa kutengwa katika hospitali za umma wasiwaambukize wengine.
Mbali na kukataa kumeza dawa kulingana na ushauri wa daktari, ni watu wachache wanaojua kwamba ni kosa la jinai kumwambukiza mtu ugonjwa wowote makusudi.
Wanaowaambukiza watu Ukimwi, wakielewa bayana kwamba wanaugua maradhi hayo wanaweza kufungwa jela.
Dkt Kiingati asema sheria hiyo ililenga kudhibiti uambukizaji wa Ukimwi makusudi .
Anasema kwamba ni kinyume cha sheria kwa mtu kumwambukiza mwingine ugonjwa wowote akielewa kwamba anaugua.
“Sio Ukimwi pekee. Ni kosa la jinai linalobeba hukumu nzito kwa mtu kumwambukiza mwingine ugonjwa anaoelewa bayana kwamba anauugua,” asema na kuongeza kuwa sheria hii inafanya kazi katika nchi nyingi duniani.
Hii ni sheria ambayo imekuwa ikiwafunga wabakaji wanaowaambukiza waathiriwa Ukimwi.
Kwa kuzuia kuenea kwa magonjwa ya kuambukizana, mabaraza ya miji yaliweka sheria kali kuzuia watu kutema mate na kikohozi katika mitaa na barabara za miji.
“Ni watu wachache wanaofuata kanuni za afya zilizowekwa na baraza la jiji. Baadhi ya watu wanakojoa katika maeneo yasiyoruhusiwa na tunawashtaki tukiwapata. Hata hivyo, ni vigumu kupambana na utemaji mate na kikohozi ovyoovyo kwa sababu askari wa baraza ni wachache ikilinganishwa na idadi ya wakazi wa jiji,” asema afisa mmoja wa idara ya mazingira katika baraza la jiji la Nairobi.
Hata ingawa kifungu kuhusu uavyaji mimba kilizua joto wakati wa kampeni za Katiba, huenda sio Wakenya wengi wanaofahamu kwamba ni kosa la jinai kutoa mimba kwa hiari bila ushauri wa daktari aliyehitimu.
Wanawake wengi wamekuwa wakitoa mimba chini ya wataalamu bandia.
Kulingana na wakili mmoja jijini Nairobi, sio mtoaji mimba pekee anayevunja sheria mbali mtaalamu anayemsaidia kufanya hivyo huwa akivunja sheria za taaluma yake.
Sheria, asema wakili huyo aliyeomba tusitaje jina lake kwa sababu za kibinafsi, inakubali tu utoaji mimba ikiwa daktari anayemhudumia mama mjamzito, anafanya hivyo kuokoa maisha ya mama na mtoto.
“Ni sharti daktari huyo awe amehitimu na sio “wataalamu wa mitaani”,” asema wakili huyo na kuongeza kuwa wanaowashawishi wasichana kutungua mimba pia huwa wanavunja sheria.
“Wanaweza kushtakiwa kwa kushirikiana na mhusika na kumshawishi kushiriki jinai,” aeleza.
Na ikiwa idara za serikali zitakaza kamba kuidhinisha sheria za kimazingira, wavutaji wengi wa sigara watajaa katika jela za humu nchini.
Sheria ya tumbako inafafanua wazi kuwa uvutaji wa sigara unasababisha madhara kwa mvutaji na watu walio katika mazingira anayovutia.
Hata hivyo, licha ya ilani za tahadhari zinazochapishwa katika pakiti za sigara, ni watu wachache mno wanaofuata maagizo hayo.
Watetezi wa afya na mazingira wamekuwa wakilalamika kuwa sheria hii haitekelezwi kikamilifu.