Nitatembelea Jowi gerezani, baba ya Monica asema
ERIC MATARA Na BENSON MATHEKA
BABA ya Monica Nyawira Kimani, mfanyabiashara aliyeuawa, Askofu Paul Ngarama, amefichua nia yake ya kumtembelea muuaji wa bintiye Joseph Irungu, almaarufu Jowie, gerezani akirejea Kenya kutoka Amerika.
Katika mahojiano na Kenya Diaspora Media huko Seattle, Washington, Askofu Ngarama alisema amesamehe wauaji wa bintiye na akaeleza hamu yake ya kufanya mazungumzo na Jowie, ambaye mnamo Machi 13, 2024, alipatikana na hatia na akahukumiwa kifo kwa mauaji ya Monica.
“Nikirudi Kenya, nitamtembelea Jowie gerezani na kufanya mazungumzo naye kwa sababu ni kama mwanangu. Nataka hii iwe sehemu ya mchakato wa upatanisho kati ya familia tatu – ile ya Jowie, Jackie Maribe (ambaye aliachiliwa huru kuhusiana na mauaji hayo), na familia yangu,” alisema Askofu Ngarama.
“Nataka kuongoza maridhiano na kuleta familia hizo tatu pamoja. Ni lazima tuhubiri msamaha na kuacha jambo hilo litulie,” aliongeza.
Kulingana na Askofu Ngarama, msamaha ni muhimu ili kumaliza maumivu ambayo familia yake imepitia tangu kifo cha Monica mnamo 2018.
Kwa sasa, Askofu Ngarama anasomea Uzamifu katika Saikolojia Nasaha katika Full Bright Theological Seminary, Amerika, na analenga kuhitimu mwaka ujao, 2025.
Monica, ambaye alikuwa amerejea kutoka safari ya kikazi katika jiji la Juba nchini Sudan Kusini, alipatikana ameuawa katika nyumba yake iliyoko Lamuria Gardens eneo la Kilimani jijini Nairobi.
Mamake Monica, Miriam Kimani, pia yuko katika safari ya kupona na anakaribia kupata afueni baada ya hukumu ya hivi majuzi ya mahakama iliyompata Jowi na hatia na kuamuru anyongwe.
“Baada ya kupatwa na uchungu wa kufiwa na mtoto, nilimuuliza Mungu maswali mengi. Mungu aliniambia nisamehe wauaji, na hata niliandika kitabu kuhusu msamaha chenye kichwa ‘Endurance in Grief‘. Kwangu mimi, msamaha ulikuwa uamuzi mgumu zaidi kufanya, lakini ni lazima tukubali,” alisema Askofu Ngarama akitafakari uamuzi wake wa kusamehe wauaji wa Monica.
Mnamo Februari mwaka huu, 2024, Jowie alipatikana na hatia ya mauaji ya Monica, huku mpenzi wake wa zamani na mshtakiwa mwenzake, mwanahabari Jacque Maribe, akiachiliwa huru kwa kukosa ushahidi wa kutosha kumhusisha na mauaji hayo.
Katika uamuzi wake wa Machi 13, Jaji Grace Nzioka alimpata Jowie na hatia na kumhukumu kifo chini ya Kifungu cha 204 cha Kanuni ya Adhabu ya Kenya.
Jaji Nzioka alisisitiza na kufafanua jinsi mauaji hayo yalivyopangwa na kukusudiwa, pamoja na hasara kubwa iliyoipata familia ya Monica na jamii.
“Baada ya kutekelezwa kwa kosa hilo, kulikuwa na jaribio la kuficha ushahidi. Uhalifu huo ulikuwa na madhara makubwa ya kisaikolojia na kimwili kwa mwathirika na familia. Upande wa mashtaka uliitaka mahakama hii kutoa hukumu ya kifo,” alisema alipokuwa akisoma hukumu hiyo.
Jaji huyo alikataa hukumu ya kifungo cha nje akisema haingestahili wala kutimiza lolote.
Jaji Nzioka alitaja sababu za uamuzi wake, akisema mauaji hayo yalikuwa yamepangwa na kukusudiwa na wahusika hawakuacha uwezekano wa mwathiriwa kunusurika.
Jaji pia alisema hasara iliyopata familia ya Monica na jamii ilikuwa kubwa na Jowie alistahili hukumu ya kifo.