Habari za Kitaifa

Wavuvi washauriwa kutumia mbinu za kisasa kuunda maboti

April 1st, 2024 1 min read

NA ANTHONY KITIMO

HALMASHAURI ya masuala ya bahari nchini (KMA) mwaka huu (2024) itaanzisha kampeni kuhimiza wavuvi kutumia mbinu za kisasa kutengeza maboti huku sensa ya vyombo hivyo vya majini ikianza.

Shughuli hiyo inalenga kuhakikisha maboti hayo yanatengenezwa kwa vifaa ambavyo haviharibu mazingira huku serikali ikizingatia usalama ya wavuvi.

Mwenyekiti wa KMA Hamisi Mwaguya alisema kuna haja kutathmini idadi ya vyombo vya majini na ubora ili kupunguza majanga.

Bw Mwaguya alisema sensa ya mwisho iliyofanyika mwaka 2014, zaidi 22, 000 vyombo vya majini vilikuwa vimesajiliwa na serikali.

“Sensa hiyo itatusaidia kutatua baadhi ya ajali zinazotokea na kujadili na kuangalia ubora vya vyombo hivyo,” alisema.

Hata hivyo, serikali imeanzisha mikakati mpya kujenga maboti na majahazi kwa kutumia vifaa vya kisasa ili kupunguza kutegemea miti na mikoko.

Kulingana na mikakati ya serikali, inanuia kusitisha utumiaji mbao katika kutengeza vyombo vya baharini.