Makala

Tamaa ya pesa ilivyogeuka kilio kwa wakazi

April 2nd, 2024 Kusoma ni dakika: 3

NA BENSON MATHEKA

WAKAZI wa lokesheni ya Kaewa iliyoko katika milima ya Iveti Wilayani Kathiani walikuwa wakisifika kwa bidii yao katika kilimo.

Vijana waliokuwa wakimaliza shule walikuwa wakijiajiri mashambani wakipanda na kukuza aina tofauti za mboga na matunda.

Sehemu za chini za milima ya Iveti zilikuwa zikibubujika maji ambayo vijana walikuwa wakitumia kunyunyuzia mimea waliyopanda shambani.

Kutokana na juhudi za wakazi, milima hii ilikuwa imepambwa kwa kijani kibichi kila wakati.

Lakini sasa hatari kuu inawakodolea macho wakazi wa eneo hili baada ya chemichemi za maji kuanza kukauka ghafla.

Wasiwasi umetanda miongoni mwa wakazi huku vijana wakikosa ajira na njaa kutishia kuangamiza wengi.

Kukauka kwa vianzo vya maji waliyotumia kunyunyuzia mashamba kumesababishwa na uharibifu wa mazingira huku wakazi wakipapia biashara ya kukuza miti badala ya mimea ya shambani.

Miti waliyopanda wakidhani ingewakomboa kutoka kwa ufukara, imebadilika kuwa tisho kwa uhai wao kwa kuharibu chemichemi za maji.

“Tulipoanza kupanda miti hii, tulidhani kuwa ingetuletea pesa. Lakini sasa imekuwa donda ndugu kwetu, imenyonya maji yote na sasa tunaumia,” asema mzee Peter Nduya mkazi wa Kata Ndogo ya Kithia.

Kulingana na mzee huyu mwenye umri wa miaka 78 miti hii imeleta madhara kwa sababu wakazi hawajazingatia kanuni za mamlaka ya kulinda mazingira nchini.

“Watu walikuwa na hamu ya kupata pesa wakapanda miti hii kiholela karibu na mito. Badala ya kuwa baraka sasa imetuletea madhara chungu nzima,” asema mzee Nduya kwa masikitiko.

Baadhi ya miti waliyopanda ni aina mbalimbali ya mikalisti ambayo huvuta kiasi kikumbwa cha maji.

Aina hii ya miti imepandwa katika nyanda za chini za milima katika maeneo yanayochiriza maji.

Kwa wakati huu asilimia kubwa ya ardhi katika lokesheni ya Kaewa na janibu zake imekaliwa na miti hii.

Ni asilimia tano tu ya ardhi iliyoachwa kwa shughuli za kilimo cha vyakula. Na mimea ya chakula inapopandwa haikui vyema kwa kuwa kivuli cha miti hii hakiipatii nafasi ya kunawiri.

“Ni wazi kuwa tuko hatarini. Watu hawakufuata utaratibu unaotakiwa walipokuwa wakipanda miti hii,” asema mtaalamu wa masuala ya mazingira Joseph Nzola aliyestaafu kutoka idara ya misitu miaka miwili iliyopita.

Nzola anasema kuwa huenda madhara ya uharibifu wa mazingira yakaenea na kufikia maeneo yanayopakana na lokesheni hii ikiwa hatua za dharura hazitachukiliwa kurekebisha mambo.

“Kwa kawaida madhara yanayosababishwa na uharibifu wa mazingira huathiri eneo kubwa,” asema .

Anatoa mfano wa kilimo ambacho kimeathirika mno kutokana na kukauka kwa mito na chemichemi za maji.

“Mji wa Machakos na sehemu nyingi za wilaya zilikuwa zikitegemea mazao ya mboga na matunda kutoka eneo hili. Wakazi wameanza kuhisi upungufu. Vijana nao wamekosa ajira na kugeukia uhalifu. Ni masikitiko makuu,” asema Nzola.

Tayari mito iliyotegemewa na wakazi ya Kwangulu, Isyukoni na Kwa Mbiti imeanza kukauka huku kiwango cha maji kikipungua kwa kasi mno.

Kwa miaka mingi mito hii imekuwa ikiwapatia wakazi maji ya kunyunyunzia shambani na ya kunywesha mifugo wao.

Fred Nzai ambaye kwa miaka mingi amekuwa akiendeleza kilimo cha mboga na matunda anasema kuwa aliamua kutafuta kazi mjini Machakos baada ya hali kubadilika.

“Maji yamepungua kwa kasi. Miti nayo inafanya mimea ninayopanda isikue vyema. Nimeamua kuelekea mjini kutafuta kibarua,” asema Nzai aliye baba ya watoto watano aliyesifika kwa kukuza aina tofauti za mboga na matunda katika eneo la Nzaikoni.

Nzai anasikitika kuwa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa na serikali kurekebisha mambo.

Kulingana naye, huenda afueni isipatikane kwa kuwa hakuna shirika lolote la kutetea mazingira katika eneo hili.

Na maafisa wa serikali ambao wangekuwa katika mstari wa mbele kuwahamasisha wakazi wanahusika katika upanzi wa miti hii.

“Wengi wao wana mashamba makubwa ya miti. Kwa hivyo sioni wa kutukomboa,” asema.

Hata hivyo , aafisa wa mazingira Kathiani wanasema kuwa hawastahili kulaumiwa kwa kuwa  wakazi walikaidi ushauri tangu mwanzo.

Afisa mmoja aliyeomba asitajwe jina alisema miti ya eucalyptus huwa haina madhara yoyote ikipandwa katika maeneo yanayostahili.

“Kwa kawaida miti hii hupandwa katika sehemu za juu za milima mbali na mashamba yanayokuzwa vyakula. Haipaswi kupandwa kwa wingi karibu na mito au chemichemi za maji,” aeleza na kuongeza kuwa wakazi wa Kaewa wanavuna matunda ya kukiuka kanuni.