Habari za Kitaifa

Mafuriko yaja – Idara ya Utabiri wa Hali ya Anga yaonya

April 1st, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA CHARLES WASONGA

IDARA ya Utabiri wa Hali ya Anga imewataka Wakenya kujiandaa kwa mafuriko katika maeneo sita nchini.

Katika utabiri wake wa hali ya anga kipindi cha mwezi mmoja kati ya Aprili 2 hadi Aprili 8, 2024, idara hiyo inasema mvua kubwa itashuhudiwa kote nchini.

“Tarajia mvua kubwa kote nchini; haswa katika nyanda za juu za Kati mwa Kenya, Magharibi mwa Kenya, Bonde la Ufa, Pwani, Kaskazini Mashariki na maeneo Kaskazini Magharibi. Watu wajiandae kwa mafuriko katika maeneo kama haya,” Idara hiyo ikasema Jumatatu, Aprili 1, 2024 kwenye ujumbe katika akaunti yake ya mtandao wa X.

Aidha, mvua kubwa itashuhudiwa katika maeneo kadha ya Nairobi na viunga vyake pamoja na Nyanza.

Tayari maeneo hayo yamekuwa yakishuhudia mvua siku chache zilizopita.

Hata hivyo, kulingana na idara hiyo, kaunti za Kaskazini mwa Kenya na zile za Pwani zitashuhudia hali ya joto jingi.

Kaunti hizo; Mombasa, Kwale, Kilifi, Lamu, Tana River, Garisaa, Isiolo, Wajir, Mandera, Marsabit na Turkana zitashuhudia kiwango cha juu cha joto cha nyuzi joto, 30 sentigredi.

Wakazi wa maeneo haya wameshauri kunywa maji kwa wingi.