Migomo ya madaktari na matabibu inayoendelea ni tishio kuu kwa nchi
MGOMO wa madaktari unaingia wiki ya tatu huku Wakenya wakiendelea kuteseka kwa kukosa huduma za matibabu katika hospitali za umma. Kauli za serikali ya kitaifa na za kaunti ni kwamba haziko tayari kutimizia madaktari matakwa yao yalivyo na hivyo basi, wagonjwa wataendelea kuteseka.
Sawa na kuongeza pilipili kwenye kidonda, maafisa wa utabibu wameanza mgomo wao wakilalamikia masuala sawa na ya madaktari.
Hii inamaanisha kuwa huduma za afya kote nchini, kuanzia mashinani hadi hospitali za rufaa zimekwama.
Wale walio na uwezo watawapeleka wagonjwa wao katika hospitali za kibinafsi huku maskini wanaotegemea hospitali za umma wakibaki na machungu yao.
Vifo havitaepukika kwa sababu kuna watu wanaotegemea huduma kutoka hospitali za umma zinazotolewa na madaktari na matabibu wanaogoma.
Watu wanaosafishwa damu mara mbili kwa wiki wako hatarini zaidi sawa na wale wanaopokea matibabu ya saratani na wanaohitaji upasuaji wa dharura au hata uliopangwa.
Licha ya hali hii, serikali inachukulia mgomo huu kuwa suala la kawaida la kuzungushana na madaktari huku ikitisha kuwafuta kazi wasiporudi kazini.
Inasikitisha kuwa hakuna upande unaohurumia wagonjwa hali inayohuzunisha chini ya utawala unaodai kwamba umejitolea kufanikisha mpango wa Afya kwa Wote.
Utekelezaji wa mpango huo hauwezekani katika mazingira ya sasa ambayo wahudumu wa afya wanaopaswa kuufanikisha wanalalamikia matakwa yao kutozingatiwa.
Huu ndio wakati mzuri kwa serikali kudhihirisha kuwa imejitolea kufanikisha mpango huu.
Hili si suala la kuachiwa serikali za kaunti pekee kwa kuwa mpango huo uliasisiwa na serikali ya kitaifa. Kufikia sasa, hali si nzuri na hakuna ishara kwamba mpango huo utafanikiwa.