WALTER ORANDO: Mwanasoka wa UoN anayepania kuwa Messi wa Tusker FC
Na PATRICK KILAVUKA
Kuwa mchezaji wa kandanda kunahitaji wewe kujitolea mhanga, kuchongwa na kujipiga msasa kupitia mazoezi ya kila mara. Pasi na kufanya hivyo, mambo husalia kuwa mwanasoka kifaa butu! Fauka ya hayo, nidhamu na kutambua talanta yako ni njia bora ya kuafikia malengo yako katika taaluma ya kabumbu.
Hii ni kauli ya straika Walter Orando, 23, ambaye mapenzi yake katika fani ya kandanda yamempelekea kucheza soka na timu mbalimbali za mtaani na zile zinashiriki katika ligi mbalimbali.
Orando alianza kuguza gozi tangu akiwa na miaka minne akiwa shule ya Msingi ya Chuo kikuu cha Moi, Chapkoilel.
“Niliaminiwa nafasi ya winga wa kulia nikiwa shule ya msingi. Lakini niliposajiliwa shule ya upili, kocha wangu aliamua kunichezesha kama difenda namba mbili kutokana na mbinu zangu za kudhibiti wavamizi wapinzani,” asema mwanasoka huyu ambaye alijiunga na Shule ya Upili ya Wavulana ya Chavakali na mkufunzi wake akampa nafasi kikosini kama beki wa kulia.
Akiwa shule ya msingi, alichaguliwa hadi kiwango cha Kanda, Uasin Gishu na kuiwakilisha katika michezo ya shule za msingi.
Mwaka wa 2012 alikuwa kapteni wa timu ya shule ya upili na hata alikiongoza kikosi cha shule kushiriki katika mashindano ya kipute cha Copa Coca Cola ambapo walifika fainali na kunyofolewa na Shule ya Wavulana ya Ambira, Kisumu.
Isitoshe, chini ya unahodha wake, timu ya sekondari alikosomea ilifika tena katika fainali za mashindano ya Aspire Football Dreams Afrika Mashariki ambayo yaliandaliwa nchini mwaka 2012.
“Tulianzia kiwango cha wilaya (kaunti ndogo), mkoa (Kaunti), kitaifa na yale ya Afrika Mashariki ambayo yaliandaliwa uga wa Kasarani,” alieleza Orando ambaye alichezea pia timu za mtaani kama Estate Football Academy Under- 14 akiwa anaishi Eldoret na ya wasiozidi miaka kumi na saba ya Olympic Football Academy, Kakamega.
Baada ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi anakosomea masuala ya Uhandisi wa Tarakilishi, alibahatika mithili ya mtende kusajiliwa na timu ya makinda wa Under – 19 wa Tusker FC.
Chuoni, anasakatia gozi timu ya Chuo Kikuu cha Nairobi kama mshambulizi.
Katika mashindano ya Shirikisho la Mchezo ya Vyuo Vikuu Nchini la Nairobi Kusini (NASOKUSA), ameifungia kikosi chake magoli mawili kutokana na michuano mitano na kuchangia mabao mengine ya timu.
Kando na kucheza timu hii, pia amejumuishwa katika kikosi cha mibabe wa chuo hiki UoN ambacho kimekuwa kikipepeta soka ya Ligi ya Kanda ya Shirikisho la Soka Kenya Kanda Tawi la Nairobi Magharibi (FKF NWRL) na kimefanya kweli baada ya kutawazwa mabingwa wa mwaka 2018 baada ya kuzoa alama 68 baada kushika dimbani mara 30.
“Nilifunga magoli sita katika ligi hiyo na kuchangia mengine kutiwa kimiani. Nimefurahia kushiriki katika ligi hiyo ambayo ilikuwa na ushindani mkali na nikajifunza mawili matatu ya kuimarisha ujuzi wangu. Kutangamana na wachezaji mbalimbali na kubadilishana mawazo kuhusu kabumbu, kulikuwa kwa manufaa kwangu,” alisema mwanadimba Orando ambaye anavuta rada ya kucheza katika ligi za hadhi nchini na hata za kimataifa.
Chini ya kocha Joseph Ouma ambaye ni mkufunzi wa soka sogora Chuo Kikuu cha Nairobi, anasema mchezaji huyu mara yake tu ya kwanza kuingia uwanjani baada ya kujiunga na chuo kikuu, akiwa mwaka wa kwanza, alijiunga na timu kufanya mazoezi.
Aliziona dalili za yeye kuwa na kipaji adimu ndani mwake na akaamua liwe liwalo atahakikisha kwamba ameamusha ari yake ya kusakata boli ili, ndoto yake ya kusoma na kucheza kanadanda itimie.
“Kwa mara kwanza kufanya mazoezi, nilitizama pasi zake, uchongaji krosi, mpira wa ikabu, mbinu yake za kumiliki mpira, ukakamavu wake, chenga na geresha zake na nikajipa moyo kwamba, tayari nimempata mchezaji ambaye nikimpiga msasa atakuwa mwanasoka wa kuiletea chuo shime. Nilikuwa radhi hata kumchezesha na nilifurahia kwani, mchezo wake ulikuwa unaimarika kila uchao,” alieleza mwalimu wa soka Ouma ambaye anatambua bidii yake kikosini na kujituma kwake akiwa mfumaji na kumchangia magoli ya timu.
Kocha Ouma anasema fomu yake kwa sasa anaona ikimpatia nafasi hata timu tajika nchini.
Kama mchezaji aliye na kiu ya kupanda majukwaa ya soka, mwanakandanda Orando anadokeza kwamba, furaha yake ni siku moja ataichezea timu ya AFC Leopards kabla kuelekea majuu kusaka majani mabichi.
Upande wachezaji ambao huwawazia sana na kuwa na matamanio ya kusakata boli kama wao ni kiungo Francis Kahata wa Gor Mahia au Lionel Messi wa Barcelona kwa sababu anaamini vipaji vyao ni halisi na adimu kutokana na jinsi wanavyomaliza mchezo kwa kuvutia sana.
Hatimaye, mwanakabumbu Orando angependa Shirikisho la Kandanda nchini kuwa na njia ambazo zitawezesha kustawishwa kwa shule za soka nchini almaarufu Akademia kama njia ya vichochea vipawa vya soka nchini ili, miaka ijayo timu ya kitaifa na timu za Ligi Kuu Nchini KPL zipate visima vya kuchota wanasoka ambao watakuza kandanda na kushiriki katika madimba kama AFCON na la Dunia.