Kilio katika ngome za Uhuru na Raila
Na VALENTINE OBARA
NGOME za kisiasa za Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa Chama cha ODM Raila Odinga zinaongoza kwa idadi kubwa zaidi ya wananchi ambao wametaja mwaka huu wa 2018 kuwa mgumu zaidi kwao kiuchumi.
Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti uliofanywa na shirika la Trends and Insights For Africa (TIFA), eneo la Nyanza, ambalo ni ngome ya Bw Odinga linaongoza kwa asilimia 67 ya Wakenya waliosema 2018 ulikuwa mwaka mgumu kwao kiuchumi ikiwa na asilimia 67, ikifuatwa na ngome yake nyingine ya Pwani kwa asilimia 61, na eneo la Mlima Kenya (asilimia 59) lililo na wafuasi wengi wa Rais Kenyatta.
Matokeo hayo yanaonyesha kuwa mwafaka kati ya Bw Odinga na Rais Kenyatta mnamo Machi mwaka huu ulifanikiwa tu kutuliza uhasama wa kisiasa uliokuwepo, lakini haukutatua changamoto za kiuchumi hasa kwa mwananchi wa kawaida.
“Suala lililotatiza wengi ni kupanda kwa gharama ya maisha. Hii ni baada ya serikali kuweka ushuru wa VAT kwa bidhaa za mafuta na huduma za fedha. Ilibainika pia Wakenya walitaabika na jinsi wengi walivyofutwa kazi kwani kampuni nyingi ziliathiriwa na mwaka mgumu wa kisiasa wa 2017, ambao uliathiri uchumi,” ikaeleza ripoti hiyo.
Eneo la Rift Valley, ambalo ni ngome ya Naibu Rais William Ruto lilifuata kwa asilimia 57 ya wananchi waliotaabika mwaka huu, huku Kaskazini Mashariki ikiwa na idadi ndogo zaidi kwa asilimia 30 pekee waliosema mambo hayakuwa magumu sana kwao.
Kwa jumla kitaifa, asilimia 56 ya Wakenya walisema mwaka wa 2018 ulikuwa mbaya na wanaomba ukamilike haraka huku asilimia 43 wakisema ulikuwa mzuri kwao.
Changamoto kubwa iliyotajwa na waliohojiwa ni gharama ya juu ya maisha ambayo ilichangia asilimia 58 ya wananchi kutoridhika, pamoja na ukosefu wa ajira.
“Masuala haya mawili pamoja na kukosa uwezo wa kupata mikopo, na umasikini yalisababisha athari mbaya kwa maisha ya Wakenya,” ikasema ripoti hiyo ya utafiti uliofanywa kati ya Desemba 19 na 21.
Kuhusu vita dhidi ya ufisadi, Rais Kenyatta kwa mara nyingine alitajwa na Wakenya wengi kuwa katika mstari wa mbele akifuatwa na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, Noordin Haji (asilimia 69) na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai, Bw George Kinoti (asilimia 65).
Idara ya mahakama ilitajwa na asilimia 53 pekee ya Wakenya, huku idara ya polisi ikivuta mkia kwa asilimia 25 kuhusu kujitolea katika juhudi hizo za kukabili ufisadi. Wengi walisema kukamata washukiwa pekee hakutoshelezi kujenga imani ya Wakenya katika vita dhidi ya ufisadi, kwani idadi kubwa (asilimia 52) walisema wanataka kuona wahusika wakuu wakifungwa gerezani wanapopatikana na hatia.