Aibu wavuvi wawili wakiuawa kufuatia mzozo wa samaki
NA GEORGE ODIWUOR
WAVUVI wawili wameaga dunia kufuatia mzozo kutokana na uhaba wa samaki katika maji ya Ziwa Victoria karibu na ufuo wa Uwi, Kaunti ya Homa Bay.
Wavuvi katika vikundi viwili walikorofishana mnamo Jumanne mchana ambapo wawili kwenye kundi lililozidiwa nguvu walipoteza maisha baada ya kuzama majini.
Mwendeshaji boti wa kikundi kile kingine alielekeza chombo hicho kugonga cha wenzao, hali iliyosababisha kuyumba.
Akithibitisha, Chifu wa Gembe Kaskazini Charles Ngoe, alisema mapigano yalianza pale wavuvi kutoka Koginga—karibu na mji wa Homa Bay, walienda Uwi na kushusha nyavu zao majini kuvua samaki.
Wavuvi wa eneo hilo hawakufurahishwa, wakiwataka wageni kuondoka kwa sababu sehemu hiyo ilikuwa ya kulea samaki wakomae.
“Wenyeji walipinga wazo hilo wakisema kwamba mahali ambapo ‘wavuvi wageni’ walishusha nyavu zao pametengwa kwa ajili ya kuwalea samaki wakomae,” Bw Ngoe alisema.
Wavuvi kutoka Koginga walipotakiwa kufungasha virago na kuondoka, walikaa ngumu.
Mapigano makali yalizuka.
“Wavuvi watano wa Uwi waliingia kwa boti yao ya doria na kuwashambulia wenzao kutoka Koginga,” Bw Ngoe alisema.
Na katika hatua ya kulipiza kisasi, wavuvi wa kutoka Koginga walitumia boti yao kugonga hii ya wenyeji hadi ikapinduka majini.
Wavuvi wote watano waliokuwa ndani ya boti hiyo walitumbukia majini. Watatu kati yao walipambana wakaelea kwa kuogelea na kuomba usaidizi lakini wawili walizama na kuaga dunia.
“Miili ya waliozama haikupatikana mara moja,” akasema chifu huyo.
Shughuli ya kutafuta miili hiyo ilisitishwa Jumanne jioni kufuatia hali mbaya ya hewa.
Bw Ngoe alilaani kitendo cha wavuvi kutoka Koginga cha kulipiza kisasi kilichosababisha vifo kisa na maana wamekatazwa eneo la ufugaji wa samaki.
“Pia walikosea kwa kugonga boti ya wenyeji, hatua iliyoishia mauti,” akasema.
Walinzi wa fuo nchini–Kenya Coast Guard Services (KCGS)– waliombwa Jumatano kusaidia katika msako wa miili ya walioangamia.
Hii si mara ya kwanza kwa wavuvi kugombana kuhusu maeneo ya uvuvi kwenye Ziwa Victoria.