Gavana alalamikia mwendo wa konokono wa miradi ya serikali kuu
VIONGOZI wa Kaunti ya Kwale wakiongozwa na Gavana Fatuma Achani, wameelezea kutofurahishwa na jinsi utekelezaji wa miradi ya maendeleo unavyofanywa polepole na serikali ya kitaifa eneo hilo.
Akizungumza wakati wa harambee ya ufadhili wa kampuni ya Tuchape Kazi Sacco Ltd katika Kaunti Ndogo ya Lunga Lunga, Bi Achani alikariri kuwa serikali ya kitaifa inafaa iharakishe kutekeleza miradi iliyoanzishwa ya kustawisha miundomsingi muhimu.
“Tunahitaji usaidizi na uingiliaji kati wa serikali ya kitaifa ili kuharakisha miradi ya maendeleo inayoendelea katika kaunti yetu,” alisema.
Mkuu huyo wa kaunti alidokeza kuwa miradi mikubwa ya miundomsingi ya kitaifa inapitia eneo hilo ambalo shughuli kuu za kiuchumi ni uvuvi, kilimo na utalii.
“Ikiwa tunaweza kuboresha miundomsingi basi itatusaidia kama serikali ya ugatuzi kuharakisha maendeleo ya kaunti yetu,” alisema.
Aliongeza kuwa miradi inayoendelea yote ni muhimu kwa usafirishaji wa bidhaa na huduma katika ukanda wa Pwani.
Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Taifa, Bw Kimani Ichung’wah, ambaye pia alikuwa katika hafla hiyo alisema serikali ya Kenya Kwanza ina nia ya kushughulikia mapengo ya miundomsingi kote nchini ili kuona uboreshaji wa sekta muhimu za uchumi kama vile kilimo, uchukuzi, nishati, afya na elimu.
Bw Ichung’wah ambaye pia ni mbunge wa Kikuyu aliwahakikishia wakazi kwamba utawala wa Kenya Kwanza utakamilisha miradi yote ya miundomsingi Kwale kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027.
Miradi muhimu inayoendelea Kwale ni pamoja na mradi wa bwawa la Mwache lenye thamani ya Sh20 bilioni, mradi wa ukarabati na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Diani uliogharimu Sh2.3 bilioni, uendelezaji wa bandari ya samaki ya Shimoni yenye thamani ya Sh2.6 bilioni, barabara kuu ya Funzi yenye thamani ya Sh1.15 bilioni kutoka barabara ya Milalani-Munja, ujenzi wa barabara ya Kwale-Kinango yenye thamani ya Sh3 bilioni miongoni mwa zingine.
Alisema serikali inayoongozwa na Rais William Ruto pia iliazimia kuvutia wawekezaji walio tayari kuingiza rasilimali katika sekta muhimu za uchumi ili kuimarisha urahisi wa kufanya biashara.
“Rais William Ruto amenituma kuwafahamisha wakazi kumpa muda wa kupata fedha za kukamilisha miradi ya miundomsingi inayoendelea kama vile barabara ya Kwale-Kinango, daraja la Mwachande na barabara kuu ya Funzi kwa wakati ufaao,” Ichungwa alisema.
Mbunge wa Lungalunga, Bw Mangale Chiforomodo, na Seneta Maalumu, Bw Raphael Chimera, pia walihudhuria hafla hiyo iliyosaidia kuchangisha Sh3.3 milioni ambazo zitasaidia kukuza kitita cha hazina ya Tuchape Kazi Sacco Ltd.