Habari za Kitaifa

BAT yataka Kenya kulegeza ilani kuhusu sigara isiyo na moshi

May 10th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

STANLEY NGOTHO Na LABAAN SHABAAN

SERIKALI imeombwa kudhibiti sekta ya tumbaku kwa msingi wa kanuni za kisayansi zilizothibitishwa kuhusu sigara bila moshi, na wala sio kuchapisha kwa pakiti ilani sawa na ya sigara ya kawaida.

Meneja Mkurugenzi wa Kampuni ya bidhaa za tumbaku ya British American Tobacco Kenya (BAT-K) Crispin Ochola anasema kampuni hiyo haipingi kanuni za serikali zinazodhibiti sekta hiyo.

“Kile tunachoamini ni kuwa bidhaa zetu zinafaa kuongozwa na kanuni. Tunaiomba Wizara ya Afya isifanye kazi kwa hisia na badala yake itoe uamuzi unaoongozwa na mchakato wa kisayansi kuhusu kanuni zilizopendekezwa,” alisema Bw Achola.

Haya yalijiri katika Kongamano la 10 la ushirikishaji umma lililofanyika katika taasisi ya mafunzo ya kiviwanda (NITA) mjini Athi River, Kaunti ya Machakos mnamo Jumatano.

Washiriki walitoka katika Wizara ya Afya, BAT-K na washikadau wengine muhimu.

Bw Ochola vilevile aliomba serikali kutoainisha bidhaa hizo za nikotini zisizo na tumbaku pamoja na sigara ya kawaida ambayo kwa kawaida huwa na asilimia kubwa ya tumbaku.

Mgogoro huu unatokana na hatua ya serikali kupendekeza maelekezo kuwa sigara na bidhaa za nikotini zisizotoa moshi zinafaa ziambatanishwe na onyo kali kuhusu madhara ya kiafya.

“Sigara isiyotoa moshi haifai kuwekewa ilani kama sigara ya kawaida. Sera bora inafaa kuonyesha madhara yaliyopungua,” akaongeza Bw Ochola.

Mwenyekiti wa Bodi ya Kudhibiti Tumbaku Nchini Bi Naomi Shaban anasisitiza kuwa kanuni hizi zinafaa kutathminiwa kulinda haki za biashara na afya ya watumiaji.

“Maoni ya Wakenya yatatiliwa nguvu wakati wa kubuni sera mpya,” alisema Bi Shaban.

Katibu Mkuu wa Shirika la kupunguza madhara la Harm Reduction Society Dkt Michael Kariuki, amerai Wizara ya Afya ifuate nyayo za nchi zilizostawi ambazo zimekumbatia bidhaa za nikotini zisizotoa moshi.

Wizara ya Afya imekuwa ikifanya mikutano na makongamano ya kukusanya maoni ya umma katika kaunti saba.

Kaunti hizo ni Kisumu, Uasin Gishu, Kakamega, Nyeri, Embu, Mombasa na Machakos.

Wakenya na washikadau wa sekta ya tumbaku wanaombwa kutoa maoni yao kuhusu pendekezo la ilani kali za kiafya kuchapishwa kwenye pakiti za bidhaa za tumbaku na sigara.