Habari za Kitaifa

Wabunge washtuka bodaboda huuziwa pikipiki za kawaida Sh571,000

May 10th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA EDWIN MUTAI

KAMATI ya Bunge inayohusika na masuala ya fedha imefichua jinsi watu wanaonunua bodaboda kwa njia ya mkopo wanavyoendelea kuporwa.

Bunge limeshangazwa na ufichuzi kuhusu mateso wanayopitia baadhi ya wanaokopeshwa pikipiki hizo. Imebainika kuwa, baadhi ya watu wamejikuta wakilipia pikipiki ya mkopo kwa kiwango cha hadi Sh571,000.

Pesa hizo, zinatosha kununua gari nzuri la mtumba.

Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Molo Bw Kuria Kimani ilijawa na hamaki baada ya wanabodaboda kusimulia masaibu yao jinsi walivyopoteza pikipiki zao kutokana na wizi unaominika unapangwa.

Mhudumu mmoja alisimulia jinsi pikipiki yake ilivyoibiwa baada ya kulipa Sh178,000 kwa kampuni ya Watu Credit Limited.

Alisema kampuni hiyo ilidai kuongezewa Sh121,000 kwa ajili ya kubadilisha pikipiki iliyoibiwa na baadaye ikasema ana salio la Sh178,000. Jumla ikiwa ni gharama ya Sh571,000.

Bw Gideon Ngeno, aliyedhamini mkopo kwa jamaa katika kampuni ya 15 Minutes Co. Ltd, alisimulia jinsi pikipiki hiyo ilivyonyakuliwa baada ya mmiliki kuamua kwenda mashambani akiwa na mkewe na mtoto.

Familia ya Bw Kevin Rotich ilinaswa katika eneo la Zambezi, kisha pikipiki ikachukuliwa na kuachwa wakiwa wamekwama barabarani. Alisema hawakufahamishwa kuwa pikipiki hiyo hairuhusiwi kufanya kazi nje ya miji ya Kikuyu, Thika na Kitengela.

“Mtu analipia Sh570,0000 kwa pikipiki moja na hajawahi kupata umiliki kamili wa pikipiki yenyewe. Hii ni biashara ya aina gani?,” alifoka Bw Kimani.

“Mtu analipa hadi Sh204,000, anapewa ufunguo mmoja bila kitabu cha kuThibitisha pikipiki ni yake. Pikipiki zinawekewa ufuatiliaji na kampuni ambazo zinatoa mikopo. Kisha pikipiki zao zinapotea miezi miwili kabla ya kumaliza mikopo.”

Mhudumu wa bobaboda, Kaunti ndogo ya Kajiado ya Kati Bw John Toto, alinunua pikipiki kutoka kwa taasisi ya MOGO. Alisimulia jinsi hati ya umiliki ilihifadhiwa na kampuni hiyo licha ya kumaliza malipo.

“Pikipiki yangu iliibiwa kwenye makazi yetu lakini nilikuwa nimekamilisha kulipa mkopo wangu. Nilipopigia MOGO simu, walisema mimi si mteja wao tena lakini bado wanashikilia hati yangu,” alisema.

Wanabodaboda hao walishutumu kampuni hizo na polisi kwa kukosa kurejesha pikpiki zilizoibiwa hata wakati vifaa vya kufuatilia vinaonyesha mahali zilipopelekwa. Bw Kimani na Bw Munyoro waliwahakikishia waendeshaji hao kwamba, kampuni zilizoathiriwa zitachukuliwa hatua na kufidia hasara ya pikipiki hizo.

Mwenyekiti wa Muungano wa Bodaboda nchini (KBA), Bw Charles Gichira, alieleza jinsi wanachama wake wametatizika kununua na kulipia mikopo hiyo kwa kampuni. Alisema wengi wameuawa, pikipiki zao kuibiwa kabla ya kukamilisha kulipa mkopo ili kuzimiliki.

“Baadhi ya wanachama wetu, nikiwemo mimi, tumetishiwa tunapotafuta jinsi ya kubadilishiwa pikipiki zilizoibiwa. Wengine wamezuiliwa kwa kisingizio cha kuiba pikipiki zao,” alisema Bw Gichira.

Baada ya ufichuzi huo, sasa kamati hiyo imeziagiza kampuni tano zinaoendesha biashara hiyo ya kuwapokesha watu pikipiki kufika bungeni.

Kampuni za Watu Credit Limited, Mogo Motorcycles Kenya, JoyInc Group, 15 Minutes, na My Boda zimeagizwa kufika mbele ya kamati hiyo wiki ijayo.

Mbali na kampunni hizo, kamati hiyo ya Bunge pia itataka maafisa wakuu wa Mamlaka ya Kitaifa ya Usalama wa Uchukuzi (NTSA) na Mamlaka ya Kudhibiti Bima (IRA) wafike ili kueleza kuhusu kupotea na kutwaliwa kwa pikipiki ambazo zilisalia kukamilisha kulipa mkopo kabla ya mwezi mmoja au miezi miwili.

NTSA itahitajika kutoa hati za miliki wa pikipiki hizo na jinsi zilivyobadilishwa huku IRA ikitoa mwanga kuhusu fidia ya bima kwa wamiliki.