Akili Mali

Mtambo mdogo unaoweza kuchakata kahawa hadi kilo 1,000 kwa siku

May 11th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA LABAAN SHABAAN

SI lazima mkulima wa kahawa anunue mitambo ya mamilioni ya pesa itakayotumiwa katika mchakato wa usindikaji kahawa pindi inapovunwa.

Mkulima mdogo anaweza kutumia mtambo wa Coffee Pulping Machine ambayo hutumiwa kuondoa maganda ya buni (mazao ya kahawa) ili kubaki na mbegu kwa kimombo coffee berries.

Mashine hii yenye uwezo wa kuchakata angalau tani moja ya buni kwa siku inaweza kuendeshwa kwa mkono, umeme ama hata mafuta ya dizeli.

Mtambo huu una dramu yenye miinuko mingi ambayo huzunguka na kugusana na bati la chuma.

Mgusano huu hufinya zao la kahawa na kutoa mbegu upande mmoja na maganda upande mwingine.

Mkulima wa mbuni atia buni za kahawa kwenye faneli ya mtambo wa kuchakata buni. PICHA | LABAAN SHABAAN

Mbegu hizo hutumiwa kutengeneza kahawa inayotumiwa kuwa kinywaji huku maganda yakirejeshwa shambani kuwa mbolea.

Ili mtambo huu uweze kuchakata buni za ukubwa tofauti, bati la chuma linaweza kukaribishwa kwenye dramu ama kusongeshwa mbali kidogo.

Vinginevyo, mwanya ulio kwenye faneli ya mtambo unaopitisha matunda ya kahawa unaweza kufanywa mkubwa ama mdogo.

Mtaalamu wa kilimo cha mbuni Andrew Rotich anaeleza kuwa mtambo huu ni tegemeo kwa wakulima wasio na uwezo mkubwa wa kifedha.

“Mtambo huu umeokoa familia nyingi vijijini katika maeneo ambayo hayana muunganisho wa umeme ama yanaishi maisha ya chini,” Bw Rotich aliambia Taifa Leo.

Mbegu za buni baada ya maganda kuondolewa. Mbegu hizi husagwa kuunda kahawa. PICHA | LABAAN SHABAAN

Sokoni, mashine hii huuzwa kwa angalau Sh50,000; kwa hivyo ni bei nafuu kwa wakulima wadogo.

Hata hivyo, Bw Rotich anakiri kuwa wakulima wengi wanapitia changamoto wanapohitajika kuchakata kahawa nyingi zaidi ya tani moja kwa muda mfupi kutegemea na hitaji la soko.

“Mkulima hupoteza muda mrefu anapoondoa maganda ya matunda ya kahawa kwa sababu wakati mwingi huhitajika kurudia mchakato huo kuhakikisha kila buni imeondolewa maganda,” alifichua.

“Endapo mkulima amefikiwa na umeme ama ana uwezo wa kununua mafuta ya dizeli ili kuendesha mtambo, kazi yake itakuwa rahisi,” aliongeza.

Bw Rotich anaendelea kusifu mtambo huu akisema kuwa unaweza kubebeka kutoka sehemu moja hadi nyingine kwa urahisi.

Kwa hivyo, mkulima anayeelewa biashara hii, ana nafasi ya kupata pesa zaidi kwa kukodisha mtambo kwa wakulima wengine.