Makala

Mama aliyejirusha mtoni akiwa na mtoto mgongoni azikwa pamoja na mwanawe

May 10th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

GEORGE MUNENE NA LABAAN SHABAAN

WALIZIKWA katika kaburi moja lakini ndani ya majeneza tofauti kijijini Kabiroini, Kaunti ya Kirinyaga.

Hii ni simulizi ya mama na mtoto wake waliotumbukia Mto Nyamindi mtoto akiwa amefungwa kwa leso mgongoni.

Ni tukio lililosikitisha wakazi wa kijiji hicho kilicho katika eneobunge la Gichugu.

Katika mazishi ya Mourine Wangui, 29, waombolezaji walikuwa wameduwaa wasijue kwa nini tukio hili lilifanyika vile.

Wanakijiji walishindwa kufanya kazi adhuhuri hiyo mazishi yalipofanyika kuelekea alasiri.

Licha ya kibaridi kikali, walihudhuria maziko huku machozi yakiwatiririka wakaazi pamoja na viongozi.

Wanakijiji walimsifu Bi Wangui kuwa mtu aliyewapenda watu na kuishi nao vyema licha ya kuwa mbele yao kimaisha.

“Alikuwa mnyenyekevu na aliyeelewana na watu,” mwanakijiji mmoja alisikika akisema.

“Ni pigo kubwa kwa familia na sasa ni wakati mwafaka tutilie mkazo afya ya akili,” alifunguka Bw Daniel Kibinga ambaye ni Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kaunti ya Kirinyaga.

Kwa mujibu shangazi yake marehemu, Bi Harriet Kabiru, kifo hiki kimetosa familia katika maombolezi ya muda mrefu.

“Kuna uvumi kijijini na mitandaoni kuwa familia haina furaha kabisa. Hii inafaa ikome kabisa ili familia iishi kwa amani,” alisema Bi Kabiru.

Hata hivyo familia imekiri kuwa Bi Wangui alikuwa na msongo wa mawazo kabla ya kujiua pamoja na mtoto wake.

Wazazi wamesema marehemu alikuwa mnyenyekevu, mwerevu, mchangamfu, mwadilifu na mwenye bidii.

Baba yake, Simon Munene ni mkandarasi na mama yake Irene Micere ni karani aliyeajiriwa na serikali Kaunti ya Embu.

Mauti Mtoni

Mourine Wangui, 29, aliyejirusha Mto Nyamindi, Kirinyaga, akiwa na bintiye, Precious Wairimu mgongoni. Picha|George Munene

Kifo cha mama na mtoto mgonjwa (Precious Wairimu) mwenye umri wa miaka mitano kilitendeka mnamo Jumamosi Mei 4.

Miili hii iliyoopolewa na polisi, ilipatikana kilomita kumi kutoka walipotumbukia mtoni.

Kabla ya kifo hicho, Bi Wangui alikuwa na msongo wa mawazo baada ya kukosana na mpenzi wake.

Vile vile, alipitia masumbuko kwa sababu ya kukosa ajira iliyoendana na utaalamu wake mbali na kuwa na mtoto ambaye alikuwa mgonjwa.

“Tulimlea vizuri na hakukosa chochote ila alikuwa na matatizo yake binafsi yaliyohangaisha maisha yake. Tulijaribu kumsaidia lakini alichukua mkondo ambao umetuacha hoi,” mamake alisema.

Familia yake inafichua kuwa Bi Wangui alipata ujauzito 2019 akiwa mwanachuo wa utabibu. Mchumba wake aliahidi kumuoa baada ya kumaliza masomo ya chuo.

Mtoto wake alipata ugonjwa wa homa ya uti wa mgongo uliomfanya akapooza. Bi Wangui alitumia muda mwingi kumpeleka hospitalini akikosa wakati wa kusaka kazi ya udaktari.

Masumbuko yaliongezeka baada ya kutemwa na mpenzi wake ambaye alioa mwanamke mwingine na kuzaa naye.

“Binti yangu alihisi amedanganywa na kusalitiwa na hali yake ikawa mbaya sana,” Bi Micere alisema akieleza walimpeleka hospitalini kwa tiba ya afya ya akili sababu wakati mwingine angepiga nduru ovyo ovyo.

 Bi Micere anafichua kuwa ulifika wakati binti yake alianza kuwa na mawazo ya kujiua baada ya kukataa dawa alizopendekezewa na madaktari.

“Wakati mwingine angenyamaza sana kutishia kuwa ataondoka nyumbani. Alipojaribu kuondoka usiku mmoja, nilimpokonya mtoto na mume wangu akaongea naye akatulia,” aliongeza Bi Micere.

Inashukiwa kuwa hatua ya Bi Wangui kuomba kupewa shamba la kahawa ajitegemee ilikuwa mpango wa kujiua.

Jumanne iliyopita, baba yake alimpa shamba ambapo Bi Wangui alipanda miti mipakani.

Siku hiyo, aliomba kuwatembelea nyanya na babu – Fridah Njoki, 80 na  Ngobo Kuruma, 90 –   Kabiroini na akaandamana na baba yake.

Siku chache baadaye, Bi Wangui alijiua pamoja na mtoto wake.