Fulham yakosea Arsenal pakubwa kwa kulimwa 4-0 na Man City
Na MWANGI MUIRURI
MATUMAINI ya Arsenal kuchukua taji la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) yameanza kufifia katika dakika ya 13 ya mechi ya Manchester City dhidi ya wenyeji Fulham ugani Craven Cottage.
Mchezaji Josko Gvardiol wa Man City ndiye alikuwa wa kwanza kuzititiga nyavu za Fulham katika mtanange huo.
Badala ya Man City itosheke na kusononesha nyoyo za mashabiki wa Arsenal kwa goli hilo moja, kunako dakika ya 59, Philip Walter Foden aliongeza la pili.
Huku matumaini yakiwa bado yako lakini hafifu, Gvardiol alirejea kwa kupachika goli la tatu katika dakika ya 71.
Mashabiki wa Arsenal walidai kwamba hilo la tatu lilikuwa la haramu ya kuotea, lakini likasimama kuhesabiwa.
Penalti dhidi ya Fulham katika dakika ya 90+6 iliyofungwa naye mchezaji Julian Alvarez ilizika matumaini hayo ya Fulham kufanya mambo katika kaburi la sahau.
Hata hakuna haja ya kurejelea takwimu za mechi hiyo, cha maana kujua ni kwamba Fulham ililemewa kwa kila safu.
Ni kama sasa Man City inaelekea kuvishwa mkufu wa ubingwa kwa mara ya nne mfululizo na ya sita kati ya misimu saba tangu msimu wa 2018/19.
Licha ya maombi ya dhati ya wafuasi wa Arsenal na Liverpool kuitakia Man City mkosi wa kupoteza mchezo huo, goli hilo liliingia kama hali ya kidonda kikavu kukwaruzwa kwa msumari na kisha kuwekwa chumvi.
Ni goli ambalo hatimaye lilirusha Man City hadi juu ya jedwali ikiwa na pointi 85 huku Arsenal iliyokuwa inaongoza jedwali hilo ikiwa na pointi 83 ikibakia ya pili sasa.
Hiyo ilikuwa mechi ya 36 kati ya zote 38 za ligi kwa Man City, sawa na Arsenal, ikiwa na maana kwamba vile kila moja yao itawania pointi sita za mwisho ndivyo itabaini bingwa wa msimu huu wa 2023/24.
Liverpool iliyo ya tatu kwa pointi 78 sasa imeaga kinyang’anyiro cha ubingwa kwa kuwa hata itekeleze maajabu gani na mangapi katika mechi zake mbili zilizosalia, inaweza tu ikamaliza katika jedwali kwa pointi 84.
Matokeo hayo ya Man City dhidi ya Fulham yanamaanisha kwamba Arsenal na Liverpool huenda zijipate katika vita vya kumaliza katika nafasi ya pili.
Hata hivyo, ni vyema ieleweke kwamba Arsenal inaweza ikamaliza ikiwa bingwa au nafasi ya pili au ya tatu.
Man City imebakisha udhia na timu za Tottenham Hotspur na West Ham United huku Arsenal ikiwa na kibarua dhidi ya Manchester United na Everton.
Nayo Liverpool itamaliza udhia wa kusaka pointi sita za mwisho dhidi ya Aston Villa na Wolves.
Iwapo kila mojawapo ya hizi timu tatu itashinda mechi zake zote kama ilivyo kawaida ya nia, basi Arsenal kwa mara ya pili mfululizo itamaliza katika nafasi ya pili, hali ambayo ni stori ambazo mashabiki wake wanaweza wakalipia kuepukana nazo.