Mafuriko: WHO yawataka Wakenya kuwa waangalifu kuepuka maambukizi
NA CHARLES WASONGA
SHIRIKA la Afya Duniani (WHO) limewashauri Wakenya kuwa waangalifu kwa sababu taifa linakumbwa na hatari ya mkurupuko wa magonjwa yanayosambaa kupitia maji na chakula kichafu kutokana na mafuriko yanayoshuhudiwa nchini.
Kwenye taarifa Jumamosi, WHO ilithibitisha kuwa visa 44 vya kipindupindu vimeripotiwa katika Kaunti ya Tana River, mojawapo ya kaunti zilizoathirika zaidi na janga hilo.
Kulingana na takwimu za hivi punde zilizotolewa na serikali, jumla ya watu 286,000 wameathirika na janga hilo, familia 54,837 zikipoteza makazi na watu 257 wakiaga dunia.
Serikali, kupitia Wizara ya Afya, imeweka mpango wa kufuatilia mikurupuko ya magonjwa wakati wa msimu kama huu wa mvua za masika.
WHO pia imenunua karibu vifaa 87 vya kudhibiti kipindupindu na vifaa 20 vya kuzuia msambao wa ugonjwa wa nimonia na ambavyo vinasambazwa kwa kaunti zilizoathirika zaidi na mafuriko. Vifaa hivyo vinaweza kuwafaa karibu watu 10,000.
“WHO itaendelea kupiga jeki mikakati ya dharura ya kuzuia mikurupuko ya magonjwa ambayo yanaweza kuenea kwa haraka,” akasema Dkt Abdourahmane Diallo, ambaye ni mwakilishi wa WHO nchini Kenya.