Dimba

Arsenal ilivyosubiri miaka 26 kuitandika Man United nyumbani na ugenini katika msimu

May 13th, 2024 2 min read

NA LABAAN SHABAAN

ARSENAL imepiku hasimu wake Manchester United maradufu kwa mara ya nne katika Ligi Kuu ya Kandanda Uingereza (EPL). Hii ni baada ya the Red Devils kuduwazwa nyumbani Old Trafford 1 – 0.

Ni mara ya kwanza the Gunners kuichapa United nyumbani na ugenini tangu mwaka wa 1998. Vijana wa kocha Mikel Arteta waliwahi kushinda wale wa Erik ten Hag walipogaragazana katika misimu ya 1997-98, 2001-02 na 2006-07.

Bao la dakika ya 20 la mshambuliaji Leandro Trossard liliwakabidhi the Gunners ushindi wa 27 msimu huu wa EPL na kufanya United kushindwa mara 19 katika mashindano yote ya msimu huu.

Arsenal walegevu lakini walishinda

Ushindi wa Arsenal ugani Old Trafford mnamo Jumapili ulikuwa muhimu sana waking’ang’ana kunyanyua kombe la EPL kwa sababu sasa wako juu ya jedwali.    

Vijana wa Arteta walikuwa walegevu lakini bado waling’aa dhidi ya wenzao wa ten Hag wakitengeneza nafasi nyingi za kucheka na nyavu.

Arsenal ilitikisa uzi katika kipindi cha kwanza baada ya Kai Havertz kupata fursa murua ya kuepuka ulinzi wa United.

Mjerumani huyu akikimbia na mpira hadi kisandukuni kabla ya kummegea Mbelgiji Trossard aliyefunga bao rahisi kwenye kimia kilichokuwa wazi.

Japo Manchester United walionekana kama wana matumaini ya kupata angalau sare, juhudi za Alejandro Garnacho ziliambulia patupu mara kadhaa.

Mchezaji wa akiba na nguvu mpya aliyetoswa ugani Gabriel Martinelli nusura azidi kutonesha kidonda cha the Red Devils alipopiga chenga na mkiki safi lakini kipa Andre Onana alikuwa macho.

Licha ya ten Hag kutumia silaha zote alizokuwa nazo kibindoni, Arsenal walibaki thabiti hadi dakika ya mwisho na kuruka hadi juu ya msimamo wa ligi.

Viongozi wa ligi watakabana koo na Everton siku ya mwisho ya msimu United (walio katika nafasi ya 8) ikishuka dimbani kukabiliana na Newcastle Jumatano.

‘Mustakabali wa Kombe la EPL U mikokoni mwa Manchester City’

Arsenal inaongoza kwa pointi 86 dhidi ya Manchester City wenye pointi 85 wakisalia na mechi mbili kukamilisha kampeni ya 2023-24.

Wachambuzi wa kambumbu wanaamini mechi ya Jumanne usiku kati ya Tottenham na Manchester City itaamua nani mkali kati ya the Cityzens na the Gunners.

Iwapo vijana wa Pep Guardiola watawaduwaza vijana wa Angelos “Ange” Postecoglou Jumanne, watafungua uongozi wa alama mbili kabla ya kushiriki mechi ya kufa na kupona Jumapili.