Kasisi aliyeanza maisha kama muuzaji changarawe akapanda hadi Askofu Msaidizi
GEORGE MUNENE NA LABAAN SHABAAN
MVULANA mnyenyekevu aliyelelewa vitongojini amekiuka mipaka na kuwa Askofu Msaidizi katika Dayosisi ya Kianglikana ya Mbeere.
Kuimarika kimaisha kwa Dkt John Kimani Nthiga kulimhitaji awe mwenye azimio lililojikita katika ukakamavu.
Aliwahi kuwa muuzaji changarawe lakini sasa yeye ni Kasisi Mkuu katika mojawapo ya makanisa makubwa nchini.
Dkt Nthiga, mkristo shupavu, alitawazwa kuwa Askofu Msaidizi wa kwanza wa Dayosisi ya Mbeere mnamo Jumapili.
Hafla hiyo ilivutia Naibu Rais Rigathi Gachagua, maaskofu kumi na sita, Wabunge na mamia ya wakazi kutoka eneo pana la Mbeere.
Kulikuwa na shangwe Dkt Nthiga alipokula kiapo cha kazi katika hafla iliyoongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Kianglikana Jackson Ole Sapit kanisani St Peters, Siakago katika eneobunge la Mbeere Kaskazini, Kaunti ya Embu.
Maaskofu wenye tabasamu tele walimkumbatia Dkt Nthiga na kumkaribisha katika himaya ya wakuu wa kanisa.
Dkt Nthiga alizaliwa mwaka wa 1969 katika kaunti Ndogo ya Mbeere Kusini alipopambana na kila aina ya changamoto na kuzikiuka.
Alivumilia jua kali na mavumbi barabarani alipotembea umbali mrefu kwenda shuleni. Hilo halikumzuia kutimiza ndoto yake.
Kiongozi huyu wa dini alizaliwa wa sita katika familia ya ndugu wanane. Alijiunga na Shule ya Msingi ya Kirima mnamo 1977 na kufanya mtihani wake wa shule ya msingi wa KCPE mwaka wa 1986.
Mwekahazina wa kikundi cha kuuza changarawe
Kisha alisajiliwa katika Shule ya Sekondari ya Kegonge na baada ya kuhitimisha kisomo hicho, alijiunga na shirika la kijamii la Kamugongo ambalo lilikuwa linauza na kusafirisha changarawe. Alifanya kazi kama mwekahazina wa kikundi hicho kwa miaka mitatu.
Akiwa katika biashara ya mchanga, Dkt Nthiga alikuwa kijana mwenye bidii kanisani. Alikuwa katibu na mwenyekiti wa Kanisa la Kianglikana la St Luke katika Parokia ya Kirima.
Ingawa alikuwa mkristo aliyebatizwa, alikuwa na ndoto ya kuwa mwanajeshi wa Idara ya Ulinzi nchini (KDF).
Shauku yake ilimsukuma kujaribu bahati yake mara tano ili ajiunge na KDF lakini hakufua dafu. Akiweka thabiti dhamira yake, Dkt Nthiga hakuacha azma ya kufana maishani.
Aliweka pembeni wazo la kuwa mwanajeshi na kupalilia ari ya kuhudumu kanisani akiamini Mungu hakumwita kuwa mwanajeshi.
Alisajiliwa katika Chuo cha St Andrew’s College for Theology and Development, Kabare. Hapa, alipopata cheti cha stashahada (diploma) na kutawazwa 1996 kuwa Shemasi (Deacon) ambaye baadaye alipewa kazi ya kasisi katika Parokia ya Ciangera.
Mwaka 1999 alitawazwa na kuwa padri kisha akapanda daraja na kuwa katibu wa utawala wa dayosisi.
Baadaye alirudi shuleni kusoma stashahada ya juu ya misheni ya mjini. Bila kukata tamaa, aliongeza kozi ya Shahada ya Sanaa ya Uongozi wa Kimataifa wa Mjini kabla ya kufuzu na Shahada ya Uzamili katika taaluma hiyo hiyo. Isitoshe aliendelea na kupata Shahada ya Uzamifu.
Dkt Nthiga ana mke na watoto wawili.
Amiminiwa sifa
Viongozi walimsifu Askofu Msaidizi wakisema ni mtu mwenye maono makubwa.
Akimpongeza Dkt Nthiga, Naibu Rais alisema askofu ni mfano bora kwa wengi wenye nia ya kufaulu maishani kijijini mwake na katika maeneo mengine ya nchi.
“Alikuwa kasisi wangu na ninajua kuwa atafaulu kwa chochote anajaribu kufikia,” alisema Mbunge wa Mbeere Kusini, Bw Nebart Muriuki.
Dkt Nthiga aliahidi kuwasaidia watu wenye mahitaji katika jamii.
“Kwa ajili ya Kristo na uwezo wa Mungu nitasaidia maskini na watu nisiowajua katika jamii,” aliapa.
“Wasaidie walio dhaifu, waponye wagonjwa, wape nguvu waliokufa moyo, watafute waliopotea,” Askofu Mkuu Ole Sapit alimwambia Dkt Nthiga.