Habari za Kitaifa

Mahangaiko ya nauli kupanda wanafunzi wakirudi shuleni

May 14th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

SHUGHULI za uchukuzi wa abiria kwa siku ya pili mfululizo zimetatizika katika maeneo mengi ya nchi wenye magari wakiunda faida ya kusafirisha wanafunzi hadi shuleni kwa nauli zilizoongezwa hadi kwa asilimia 100.

Maeneo mengi ambayo nauli huwa za kati ya Sh50 na Sh600 kulikuwa na ada mpya za kati ya Sh100 na Sh1,200 huku masafa marefu ya kati ya Sh1,000 na Sh1,500 kulikuwa na mpya kati ya Sh2,000 na Sh3,000.

Katika maeneo mengi ya Mlima Kenya, abiria walikwama kwa barabara magari mengi yakiwa katika biashara ya kusafirisha wanafunzi.

“Tumeshuhudia wingi wa watu katika steji na kama kawaida ya ilivyo hali ya wingi wa abiria lakini magari yakiwa machache, nauli hupanda,” asema mwenyekiti wa wamiliki magari wa Mlima Kenya Bw Micah Kariuki.

Bw Kariuki alisema kwamba kwa sasa hali inatazamiwa kurejea ya kawaida kuanzia Jumamosi.

“Nauli ya juu isiwajalishe kwa kuwa ni hali ya misukumo ya kibiashara. Hali itarejea kuwa ya kawaida baada ya wanafunzi wote kuripoti shuleni. Ni sawa tu na jinsi wafanyabiashara wanavyouza bidhaa zao kwa bei za juu wakati kuna upungufu sokoni,” akasema.

Mbunge wa Maragua Bi Mary wa Maua aliteta kwamba “barabarani nilishuhudia mahangaiko ya Wakenya wakitafuta namna ya uchukuzi huku wanafunzi waliokuwa na sare rasmi za shule wakiwa miongoni mwao”.

Alisema kwamba kuna taswira ambapo kuna Wakenya ambao hawajali kuwa na moyo wa kusaidia kupunguzia wenzao mahangaiko ya kimaisha.

“Mimi nilibeba wengi iwezekanavyo. Nilitegemea Wakenya wengine walio na magari yao ya kibinafsi wasaidie. Lakini sio wengi walichangamkia hali hiyo. Hii tabia ya wengine wetu kutokuwa na moyo wa kusaidia sio njema hata kidogo,” akasema Bi Wa Maua.

Mwenyekiti wa muungano wa wazazi katika ukanda wa Mlima Kenya Mashariki Bi Susan Kariuki alisema kwamba hali ni ngumu ajabu.

“Wametuongezea nauli. Wametuongezea karo. Bei ya vitabu imepanda na zile pesa za matumizi ambazo sisi huwapa hawa watoto wetu lazima zipande. Hii ni jehanamu ya elimu,” akasikitika Bi Kariuki.

Alisema serikali inafaa kuwa makini sana na haya mambo ya ushuru na gharama ya maisha.

“Kuna shida kubwa sana na tusipochunga, hii nchi hatutapata usawa katika hali zote ikiwa tutavurugika kiuchumi kiasi cha kutoelimisha watoto wa wanyonge,” akaongeza.