Makala

Mwanamume aliyekataa kuwa padri asimulia alivyotaka kujiua mara tatu

May 15th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA FRIDAH OKACHI

MWANAMUME mmoja kutoka Waithaka, jijini Nairobi, anasema matukio ya kujaribu kujitoa uhai kwa kulazimishwa kuwa padri hayajafutika akilini mwake.

Bw Stephen Kamau anakumbuka jinsi alivyokataa kufuata mawaidha ya mamake mzazi wa kumzaa kabisa aliyependelea mwanawe afuate njia ya kukua kidini hadi kuwa padri.

Ikiwa miaka imesonga tangu afanye vimbwanga hivyo, Bw Kamau anasema anajutia matendo yake, makovu mwilini yakimrejeshea matukio hayo ya kutisha.

Ingawa hivyo, mabapa na makovu mengi yalirekebishika alipopandikiziwa ngozi baada ya kujitetekeza.

Bw Kamau aliambia Taifa Leo, jaribio la kutaka kujitoa uhai kwa kujiteketeza moto lilimwacha na majeraha ya asilimia 70.

Makovu kwenye mikono ambayo Bw Stephen M Kamau alipata kutokana na jaribio la kutaka kujitoa uhai kwa kujiteketeza. PICHA | FRIDAH OKACHI

Alitibiwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH).

“Majaribio mawili yalikuwa yamekataa na hili la tatu, nilitaka niondoke machoni mwa familia yetu kabisa. Nilijifungia ndani ya nyumba yangu na kuwasha moto,” akasema Bw Kamau.

“Wakati wa tukio hilo, dadangu aliita jamaa zangu walionusuru maisha yangu na kunikimbiza hospitalini kupata matibabu,” akaongeza.

Baba huyo wa watoto wanne anaeleza kuwa akiwa hospitalini alikabiliwa na uchungu mwingi kutokana na majeraha mengi aliyokuwa amepata.

Ngozi yake ilikuwa imeathirika zaidi. Madaktari katika hospitali walilazimika kumpandikizia ngozi.

“Majeraha kwenye baadhi ya viungo vyangu kama vile mikono na miguu, hunipa kumbukumbu. Wito wangu kwa kijana yeyote awaye ni kwamba licha ya mzazi kuwa na mawazo tofauti, kijana hafai kuchukua uamuzi kama wangu,” akashauri.

Kulingana naye, jaribio la kwanza kukatiza maisha yake alifanya akiwa Kidato cha Tatu baada ya kupelekwa katika shule moja ya wavulana mjini Meru.

Kipindi hicho alitamani kuwa mfanyabiashara na sasa matumaini yake yalionekana kudidimia wakati huo.

“Unajua wakati huo, wazazi ndio walikuwa wakiamua utafanya nini. Mama aliponiambia alitaka niwe padri, nilijua anasa zangu zingefifia. Nilikereka mno,” akasema Bw Kamau.

Lakini lililomuumiza ni mamake kusisitiza kwamba ni lazima mwanawe awe padri.

“Nilipokuwa hospitalini nikiuguza majeraha nilimsikia mama akisema ‘wewe hutakuwa wa kwanza kujaribu kujiua’,” akasema.

Baada ya kuruhusiwa kuondoka hospitalini na kurudi nyumbani, wazo la kujitoa uhai likaja tena. Ndipo alifanya hivyo kwa mara ya pili na ya tatu.

Lakini, mamake Kamau, Bi Judy Wanjiru, anaambia Taifa Leo matukio hayo ya mara kwa mara yalimfanya kubatilisha kauli na msimamo kuhusu mustakabali wa mwanawe. Alihisi kuwa kitinda mimba wake alistahili kujiamulia alichotaka kuwa maishani.

“Niliona ni vyema nimuache kufanya maamuzi ya kibinafsi ambayo yangempa furaha. Sisi wazazi mara nyingine huwa na wakati mgumu kusikiliza mtoto kile anachotaka kuwa maishani. Hakuna mtu ambaye hataki mtoto wake afanikiwe. Nilipomtaka awe padre, nilijua kazi ya aina hiyo ya kumtumikia Mungu moja kwa moja ilikuwa nzuri kwake,” akasema Bi Wanjiru.

Mama huyo mwenye umri wa miaka 68, anasema kwa sasa Bw Kamau ndiye mwanawe ambaye huwa karibu sana naye kila siku pale nyumbani.

Kwa wakati mwingi Bw Kamau humshughulikia kwa mambo mengi mamake nyumbani.

“Tumesalia kuwa marafiki wa chanda na pete. Sasa hivi mwanangu huyo ndiye anajua ninafaa kula wakati upi maana nina matatizo ya kiafya,” akamsifia mwanawe.

Bw Kamau alipiga hatua maishani ambapo alisomea kozi ya ufundi wa stima.

Mbali na kazi hiyo, yeye pia ana nyumba kadha za wapangaji kulipia kodi.

Bw Stephen M Kamau kwenye mahojiano na Taifa Leo. PICHA | FRIDAH OKACHI