Jinsi mashirika yanavyohusisha vyuo kurejesha misitu
NA JESSE CHENGE
WAKATI huu ambapo athari za mabadiliko ya tabianchi zinavyozidi kujitokeza, yakiwemo mafuriko ya maafa, wanafunzi wa vyuo vikuu wanaendelea kushirikiana na mashirika kupanda miche ya miti katika misitu mbalimbali nchini.
Wiki hii, wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Masinde Muliro (MMUST) wakishirikiana na mashirika ya kuhifadhi mazingira, wanakusudia kupanda miche 200,000 ya miti katika msitu wa Kaberwa ulioko eneo la Mlima Elgon, Kaunti ya Bungoma.
Akizungumza na waandishi wa habari katika msitu wa Kaberwa, siku ya Jumatatu wakati wa uzinduzi wa upandaji wa miche hiyo ya miti, Afisa wa Masoko na Uenezi wa Shirika la mazingira la Youth for Green Action Kenya (YGAK) Teddy Ouma alisema kuwa vijana walichukua hatua ya kupanda miche ya miti katika msitu wa Kaberwa ili kuhifadhi mfumo wa mazingira ulioharibika.
Hatua zao zinalenga kusaidia msitu huo kurudi katika hali yake ya awali.
Anasema kuwa mabadiliko ya tabianchi yameathiri kila mtu na zinahitaji jitihada za pamoja kukabiliana na mgogoro huu wa kimataifa.
“Sisi kama kikundi tumefanya shughuli za kupanda miti katika sehemu tofauti za nchi kuanzia Kakamega, Narok, Kisumu, Mombasa, na maeneo mengine nchini kuhakikisha kuwa mifumo ya mazingira iliyoharibika inatunzwa na kurejeshwa kwa ubora wa awali,” alisema.
Aidha, Bw Ouma alibainisha kuwa YGAK ilichagua msitu wa Kaberwa katika Mlima Elgon kutokana na ukweli kuwa “hali yake kwa sasa inatisha”.
“Tumetembea ndani ya msitu huu wa Kaberwa ninaweza kuthibitisha kuwa ni mfumo wa mazingira ulioharibika zaidi kutokana na shughuli za kibinadamu. Tunataka kuhakikisha kuwa tunarudisha hali yake ya zamani,” aliongeza.
Alitaja athari mbaya za ukataji miti kuwa ni kukausha mito, mito kuwa midogo, na mabwawa katika eneo hilo kukosa maji.
Alisema vijana wana nia ya kusaidia serikali kufikia lengo lake la kupanda miti bilioni 15 ndani ya kipindi cha miaka mitano, na malengo ya shirika lao ni kupanda miti 1 bilioni kwa ajili ya mustakabali wa kupata mazingira matulivu.
Meneja wa msitu wa Kaberwa, Bw Godfrey Opana katika hotuba yake, alipongeza kikundi cha vijana kwa kuamua kupanda miti katika msitu huo na kusema kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo la Rais William Ruto la kuifanya nchi kuwa na misitu zaidi.
“Upandaji wa miti unapaswa kuendelea kwa miezi sita ijayo, leo (Jumatatu) kile tunachofanya ni kuendeleza kile kilichofanyika Ijumaa,” alisema Bw Opana.
Afisa huyo alisema kuwa baada ya kupanda miche 200,000 ya miti, jamii itapewa jukumu la kuitunza ambapo watapewa maeneo ya kulima huku wakitunza miche hiyo hadi ikomae.
Afisa huyo alikiri kuwa msitu wa Kaberwa umeharibika na kufichua kuwa msitu huo una eneo la hekta 1,200 ambazo zimeharibika.
Alithibitisha kuwa kwa kupanda miche 200,000 ya miti kutamaanisha kuwa “tutapunguza karibu hekta 125 kutoka kwenye hekta 1,200 zilizoharibika”.
“Hatua hii ya vijana ni faida kwetu kama kituo kwa sababu mwaka huu 2024 lengo letu ni kupanda hekta 330 ndani ya kipindi cha miaka mitatu,” alisema.
Ili kuhakikisha kuwa miti iliyopandwa inakua, afisa huyo alithibitisha kuwa kituo hicho kitawapa wakulima maeneo ambapo kila mwanajamii atapata nusu ekari baada ya kulipa ada husika.
“Jamii pia itanufaika kwa kuwa sisi pia tunazingatia wazo la Rais la kuhakikisha utoshelevu wa chakula na wakati huo huo kulinda msitu,” alisema.
Dkt Collins Matemba, msajili wa mipango, utafiti na uvumbuzi katika MMUST, alisema kuwa upandaji miti ni mojawapo ya njia za kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kuwa ni zoezi litakalosaidia eneo hilo kupata afueni.
“MMUST inashirikiana na mashirika mengine yasiyo ya kiserikali kupanda miti katika eneo hilo,” alisema Dkt Matemba.
Msajili huyo pia alisema kuwa Shirika la Misitu Nchini (KFS) limeipa MMUST lengo la kupanda miche 28,400 kwa mwaka huu wa kifedha.
“KFS imetenga ekari 100 za ardhi katika Mlima Elgon kwa MMUST kupanda miche ya miti,” aliongeza.