Habari za Kitaifa

NYS na KDF kuharakisha ujenzi wa uwanja wa Masinde Muliro Kanduyi

May 15th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA JESSE CHENGE

KATIBU wa Wizara ya Usalama wa Ndani, Raymond Omollo, amefichua kuwa serikali imetuma maafisa zaidi ya Shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) na wanajeshi ili kukamilisha ujenzi na ukarabati wa uwanja wa Masinde Muliro Kanduyi kabla ya sherehe za Madaraka Dei.

NYS na KDF sasa watashirikiana na mwanakandarasi.

Dkt Omollo alikuwa ameandamana na makatibu wenzake, Patrick Mariru (Ulinzi) na Mhandisi Peter Tum (Michezo).

Alitoa taarifa hiyo Jumanne baada ya ziara fupi katika uwanja huo ulioko Kaunti ya Bungoma.

“Sasa tumewaleta wanajeshi (KDF) ili kusaidia kukamilisha ujenzi wa uwanja. Pia watatusaidia katika usimamizi wa sehemu ya mwisho ya kazi inayoendelea,” alisema Dkt Omollo.

Katibu wa Wizara ya Usalama wa Ndani, Raymond Omollo akihutubia wanahabari uwanjani Masinde Muliro Kanduyi, Kaunti ya Bungoma mnamo Mei 14, 2024. PICHA | JESSE CHENGE

Alisema licha ya muda kuyoyoma ambapo Juni 1, 2024,  inakaribia, kazi itakamilika kwa wakati.

“Nilisema tulikuwa na kuchelewa kidogo katika kufikia muda uliopangwa ndiposa pamoja na wenzangu, tumerejea kujithibitishia wenyewe na Wakenya kuwa tumepiga hatua tangu wakati huo,” akasema.

Alisisitiza kuwa kuna maendeleo makubwa katika kukamilisha ujenzi wa uwanja huo, hasa kwenye sehemu za viti na jengo la wanaume.

“Tunataka kuwahakikishia watu wa Bungoma na nchi nzima kuwa tunaelekea kufanikisha sherehe za Madaraka Dei,” akahakikisha.

Akitoa hotuba yake, Gavana wa Bungoma, Kenneth Lusaka, alikariri kauli ya Dkt Omollo akisema kulikuwa na wasiwasi kuhusu kuchelewa kwa ujenzi wa uwanja huo, lakini sasa ni thibitisho kuwa sherehe za kitaifa zitafanyika kama ilivyopangwa.

“Tumetembelea uwanja na tumeridhika kwamba sherehe za Madaraka zitafanyika hapa. Tuwakaribisha Wakenya kutoka kila kona ya nchi wafike Bungoma ya ‘Mulembe’ mnamo Juni 1, 2024,” akasema gavana Lusaka.

Gavana Kenneth Lusaka (kulia) akiwa na Katibu wa Wizara ya Usalama wa Ndani, Raymond Omollo na maafisa wengine katika uwanja wa Masinde Muliro Kanduyi. PICHA | JESSE CHENGE