Makala

Shughuli mbovu za binadamu zakausha chemchemi za maji Bungoma

May 16th, 2024 4 min read

NA JESSE CHENGE

HUKU ulimwengu mzima ukiwa unakabiliwa na athari zisizotabirika za mabadiliko ya tabianchi, wito umetolewa kwa waja kuhakikisha wanafanya kila liwezekanalo kudhibiti hali hiyo.

Kulingana na Msemaji wa Serikali Isaac Mwaura kufikia Mei 14, 2024, takriban watu 289 walikuwa wamepoteza maisha yao kutokana na mafuriko na maporomoko ya ardhi.

Uharibifu mkubwa wa misitu katika eneo la Mlima Elgon umesababisha madhara kwenye chemchemi, mabwawa, na mito katika eneo hilo.

Aidha, mito mingi imekauka.

Taifa Leo ilimhoji Nick Lutukai, Mtaalam wa Mazingira, aliyethibitisha kuwa chemchemi za mito ya Bungoma zimekauka kutokana na shughuli za binadamu, huku uvamizi wa ardhi ya kingo za mito nao ukisababisha hali kuwa mbaya zaidi.

Bw Lutukai alieleza kuwa upandaji wa miti isiyofaa karibu na vyanzo vya maji pia umechangia ukaukaji wa mito.

Alisema uharibifu usiokoma wa misitu katika Mlima Elgon pia umeathiri maji ya chini ya ardhi.

Alitoa mfano wa bwawa la Bukokholo lililoko katika eneo la Sirisia ambalo limeathiriwa na shughuli za kibinadamu na uvamizi, huku wenyeji wakichukua ardhi ya bwawa ambapo wanaitumia kwa kilimo na malisho ya mifugo.

Bwawa la Bukokholo ambalo awali lilikuwa na ukubwa wa ekari 15, lilijengwa mwaka 1958 na Wazungu na lilizungukwa na miti ya kiasili, likiwa na jukumu la kutoa maji kwa matumizi ya nyumbani.

Mtaalamu huyo alirejelea historia kuwa baada ya kukamilika kwa bwawa hilo, lilikabidhiwa kwa serikali ya mitaa (Manispaa ya Malakisi) iliyokuwa na jukumu la uhifadhi wake.

Kabla ya uvamizi na uharibifu wa mazingira katika eneo hilo, bwawa hilo lilikuwa na jukumu muhimu katika kutoa samaki, huku wenyeji wakitumia maji kwa kilimo cha mboga, na faida nyingine.

“Kabla ya eneo hili kuvamiwa, lilikuwa linahudumia wenyeji vizuri sana, watu wangeweza kupata mboga na samaki kwa bei ya chini, lakini baada ya uvamizi na uharibifu wa mazingira, eneo hili limeharibika,” alisema Bw Lutukai.

Alibainisha kuwa sasa bwawa hilo halina uzio, maji yamepungua, na gugumaji limeenea kote.

Alibainisha kuwa kuvunjika kwa kiwanda cha Malakisi kumechangia kwa kuharibika kwa bwawa hilo.

“Kabla ya kiwanda cha Malakisi kuvunjika, eneo hili lilikuwa na shughuli nyingi,” alisema.

Bw Lutukai, hata hivyo, alisema serikali ya Kaunti kupitia wizara ya mazingira, utalii, maji, rasilimali za asili, na mabadiliko ya tabianchi imeungana na wadau wengine muhimu kulinda chemchemi za maji, lakini wenyeji bado wanang’oa miche iliyopandwa.

“Wanamazingira wanashindwa kurejesha chemchemi sababu ya rasilimali chache katika Kaunti na ndio maana tunawaomba washirika kuja na kutusaidia kurejesha vyanzo vya maji,” alisema.

Pia alifichua kuwa watu wanaoishi karibu na mito wameharibu miti ya asili karibu na mito ambayo imeleta hatari ya ukaukaji wa mito.

Alihimiza kutopanda miti ya mikalatusi karibu na mito, akionya kuwa miti hiyo sio rafiki wa maji.

“Hifadhi ya kingo za mito ni mali ya serikali, kwa hivyo watu wanapaswa kuepuka kulima karibu na hifadhi hiyo, kwani inachangia ukaukaji wa mito,” alisema.

Katika eneo la Bumula, bwawa la Kisawai lililindwa vizuri na linaendelea kutoa maji.

Meneja wa Bwawa la Kisawai Bw Hussein Barasa, alisema wamewekeza kwa kiasi kikubwa katika uhifadhi wa bwawa ambalo limegeuka muhimu kwa kuingiza kipato.

“Uhifadhi wa mazingira umekuwa shughuli inayotuingizia kipato kupitia upandaji wa miche ya miti, biashara ya samaki, mboga na matunda,” alisema Bw Barasa.

Aliongeza kuwa wenyeji wanategemea sana bwawa hilo kwa maji safi na faida nyinginezo.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Uhifadhi wa Mazingira Nchini (Nema) wa Kaunti ya Bungoma Vincent Mahiva, alisema kuwa mabwawa mengi Bungoma yamejengwa na binadamu na yanatekeleza majukumu muhimu kwa upande wa uchumi na matumizi ya nyumbani.

Aliongeza kuwa mabwawa mengi katika eneo hilo yalianza kujengwa wakati wa ukoloni kwa lengo la kuimarisha umwagiliaji na shughuli nyingine za kilimo.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa mabwawa mengi yanapatikana katika maeneo ya Tongaren, Bumula, Kimilili, Kabuchai, na Sirisia na yanatekeleza jukumu muhimu katika kuimarisha kilimo ndani ya kaunti.

Alisisitiza kuwa licha ya kuwa na mabwawa katika Kaunti, wanakabiliwa na changamoto kubwa zinazotokana na shughuli za kibinadamu zinazofanyika karibu na maeneo ya mabwawa, huku uvamizi ukitajwa kama changamoto kuu inayoathiri mafanikio ya mabwawa.

“Kwa kuongezeka kwa idadi ya watu, watu wanakaribia maeneo ya kingo za mabwawa haya, na wanapofika huko wanachangia kujaa kwa matope kutokana na matumizi ya ardhi karibu na maeneo ya kingo za mabwawa,” alisema Bw Mahiva.

Kutokana na kujaa kwa matope, Bw Mahiva alisema kuwa mabwawa mengi hayatekelezi majukumu yao kama ilivyokusudiwa.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Uhifadhi wa Mazingira Nchini (Nema) katika Kaunti ya Bungoma Vincent Mahiva. PICHA | JESSE CHENGE

Kwa kuongezea, Bw Mahiva alilalamikia viwango vya juu vya uchafuzi katika mabwawa kutokana na usimamizi duni wa taka, huku akisisitiza umuhimu wa kuhamasisha jamii kuhusu utupaji na usimamizi bora wa taka.

“Sumu ni tishio kubwa kwa viumbe wa majini, kwa hivyo tunawaomba wanajamii watupe taka yao ipasavyo,” alisema.

Bw Mahiva aliwataka wale wanaoishi karibu na mabwawa na mito kupanda spishi za miti zinazofaa kwa maji karibu na mabwawa na mito.

“Usipande miti kama mikalatusi kwa sababu wakati inapandwa karibu na mabwawa na mito hutatiza vyanzo vya maji,” alisema.

Naye mwanasayansi Robert Sawa ambaye ni mtaalamu wa rasilimali za asili, alibainisha kuwa Kaunti ya Bungoma ina asilimia 20 ya miti huku misitu ikiwa ni asilimia 14.

Aliongeza kuwa Bungoma ina mito mikubwa zaidi ya 10 na mabwawa zaidi ya 30 yaliyosambazwa katika wilaya ndogo, akisema kuwa Kaunti inakabiliwa na changamoto katika uhifadhi wa mabwawa kutokana na uvamizi katika misitu asili na ardhi ya kingo.

“Changamoto nyingine inayoathiri karibu mabwawa yote ni mazoea ya kilimo ambayo yamesababisha kujaa kwa matope katika mabwawa,” alisema Bw Sawa, akiongeza kuwa wakati mabwawa yanajaa matope, uwezo wake wa kuhifadhi maji unakuwa hatarini.

Aliongeza, “Ili kuepuka kujaa kwa matope katika mabwawa yetu, tunahimiza wakulima wanaoishi karibu na mabwawa kuunga mkono upandaji tena wa miti.”

Aidha, Bw Sawa alithibitisha kuwa serikali ya kaunti imefanya hamasisho katika jamii ili kuwaelimisha juu ya aina ya miti ambayo inapaswa kupandwa karibu na mabwawa na mito.

Mtaalamu huyo alisisitiza kuongezeka kwa shughuli za uchimbaji wa mawe na uvunaji wa mchanga karibu na mabwawa na mito kama changamoto nyingine na kuwataka watu wanaopenda shughuli haramu kufuata miongozo iliyowekwa.

“Baadhi ya machimbo hayajarejeshwa katika hali nzuri ambapo yanakuwa tishio kwa afya,” alisema.