Maoni

Ni ukatili kuongeza Wakenya mzigo ilhali tayari wanaumia

May 16th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MARY WANGARI

RIPOTI kuhusu ada mpya za ushuru zilizopendekezwa katika Mswada wa Fedha 2024 ambazo zitaongeza hata zaidi bei ya bidhaa za kimsingi, ni sawa na kutia msumari moto kwenye kidonda.

Bei ya mkate inatarajiwa kupanda kwa karibu Sh10 huku ada inayotozwa huduma muhimu kama vile kutuma pesa kupitia simu na benki zikiongezeka hadi asilimia 20, endapo Mswada huo utapitishwa kuwa Sheria.

Mswada wa Fedha 2024 umejiri huku Wakenya wakikodolea macho uwezekano wa kodi za nyumba wanazopangisha kuongezwa baada ya Mamlaka ya Kukusanya Ushuru (KRA) kuwalenga wapangishaji katika juhudi za kuongeza mapato yake.

Wapangishaji sasa watahitajika kusalimisha asilimia 1.5 ya mapato yao ya kodi kuanzia Mei 9, huku KRA ikihoji kwamba, Sheria kuhusu Nyumba za Bei Nafuu 2024 ilianzisha Ushuru wa Nyumba za Bei Nafuu kwa watu wote.

Huku hayo yakijiri, Bunge la Kitaifa linashinikiza bajeti yake ya 2024/2025 kuongezwa hadi Sh65.8 bilioni kwa lengo la kuwezesha wabunge na maseneta kutekeleza majukumu yao.

Kitita cha Sh165 milioni kwa lengo la kupamba eneo la jikoni Bungeni na Sh700 milioni za kuwezesha upeperushaji wa moja kwa moja wa matukio katika Bunge na Seneti ikiwemo kamati, ni miongoni mwa maombi yaliyowasilishwa.

Kama kwamba mzigo huo haujawalemea Wakenya vya kutosha, kuanzia Julai 1, walipa ushuru watahitajika kukaza kamba zaidi kulipa Sh1.4 bilioni katika bajeti ya 2024/2025, ili kugharamia mishahara na burudani kwa washauri wa Rais.

Hata hivyo, mkondo huu mpya wa matukio ni wa kushangaza, hasa ikizingatiwa kwamba, Rais William Ruto alitarajia bajeti ya Bunge kupungua kwa hadi Sh400 milioni katika kipindi cha 2024/2025, kufuatia ufunguzi wa jumba la Bunge Tower.

Jumba la Bunge lenye orofa 28 na lililogharimu walipa ushuru jumla ya Sh9.6 bilioni kutoka kiasi cha awali cha 5.89bilioni linasheheni afisi na vyumba vya kisasa vya mikutano vilivyodhamiriwa kuepushia Bunge gharama ya kukodisha hoteli za kushiriki mikutano.

Uhalisia ni kwamba, taifa na Wakenya kwa jumla kwa sasa wanapitia mambo mengi magumu na huu si wakati wa kuwaongezea mzigo wa ushuru wala viongozi kujipakulia minofu zaidi.

Kuna masuala mengi yanayostahili kupatiwa kipaumbele kwa sasa ikiwemo kuwapa makao wanajamii waliofurushwa na mafuriko ikiwemo kulainisha mikataba ya walimu wa JSS ambao wamegubikwa na sintofahamu kuhusu hatima yao.

[email protected]