Jamvi La Siasa

Mwanaharakati David Kimengere ajitolea kupatanisha Gachagua, Uhuru

May 16th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

NA WANDERI KAMAU

BW David Kimengere si mgeni katika masuala ya uanaharakati wa kisiasa nchini.

Alianza uanaharakati wake mnamo 1992, akiwa na umri wa miaka 14 pekee.

Je, sababu yake kujitosa katika masuala ya uanaharakati ni yapi? Alitoa msukumo huo wapi?

Kwenye mahojiano ya kipekee na Taifa Leo, Bw Kimemgere anasema kuwa lengo lake kuu ni kuona sauti ya kila mtu katika jamii—awe mkubwa au mdogo—ikiheshimiwa.

“Ni vibaya wakati sauti za watu wasioonekana kuwa muhimu katika jamii zinapodharauliwa au zinapokosa kutiliwa mkazo, ilhali zinaweza kuwa na manufaa kwa jamii,” asema mwanaharakati huyo, ambaye ni mzaliwa wa eneo la Othaya, Kaunti ya Nyeri.

Na katika nyakati hizi ambapo eneo la Mlima Kenya limekuwa likikumbwa na siasa za ushindani, hasa baina ya Naibu Rais Rigathi Gachagua, mbunge Ndindi Nyoro (Kiharu), Waziri wa Utumishi wa Umma Moses Kuria kati ya wanasiasa wengine, Bw Kimengere anasema ndiye aliyeanzisha miito ya kuwarai wanasiasa hao kuungana hata kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

“Mimi ni kama Nabii. Niliona athari za migawanyiko ambayo ilikuwepo na imekuwepo katika eneo hili kabla na baada ya uchaguzi wa 2022,” akasema Bw Kimengere.

Anasema kuwa siku 39 kabla ya uchaguzi huo, alimrai Bw Gachagua—wakati huo akiwa mgombea-mwenza wa Rais William Ruto katika mrengo wa Kenya Kwanza—kutafuta muafaka na maelewano ya kisiasa na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, ili kuhakikisha kuwa eneo hilo halikuachwa kama yatima kisiasa.

Alitoa matamshi hayo katika eneo la Othaya, wakati wa hafla ya mazishi ya mamake gavana wa Laikipia, Bw Joshua Irungu.

“Katika mila na desturi za jamii ya Agikuyu, si vizuri mzee mkongwe anapokaribia kuaga kutoa matamshi mabaya au ya hasira. Ili kumzuia kufanya hivyo, alikuwa akipewa maji ili kumzuia kufanya hivyo. Hivyo, wito wangu kumrai Bw Gachagua na viongozi wengine katika Kenya Kwanza nyakati hizo kubuni maelewano na Bw Kenyatta, haukulenga kuwashawishi kumuunga mkono Bw Raila Odinga kuwania urais, bali lengo kuu lilikuwa kuhakikisha Bw Kenyatta hakustaafu akiwa na machungu yoyote ya kisiasa kuwahusu wakazi wa Mlima Kenya,” akasema mwanaharakati huyo.

Hivyo, anasema hatua ya Bw Gachagua kushinikiza maelewano na Bw Kenyatta mnamo Machi ni “timio la utabiri wake aliotoa hata kabla ya uchaguzi wa Agosti 2022”.

Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio Machi 25, 2024, Bw Gachagua alieleza kusikitishwa kwake na matamshi yaliyotolewa na wanasiasa wa Kenya Kwanza dhidi ya familia ya Bw Kenyatta—hasa Mama Ngina Kenyatta—akiomba msamaha kutoka kwake na familia ya Bw Kenyatta kwa jumla.

Bw Gachagua pia alisema yuko tayari kufanya handisheki na Bw Kenyatta, kama njia ya “kuondoa migawanyiko ambayo imekuwa ikishuhudiwa”.

Katika hayo yote, Bw Kimengere anasema hayo yanatokana na matamshi aliyotoa.

Ikizingatiwa kwamba kufikia sasa haijabainika kuhusu ikiwa viongozi hao wawili wameafikiana kisiasa au la, Bw Kimengere anasema yuko tayari kuwapatanisha.

“Kama mzaliwa na mmoja wa wakazi wa Mlima Kenya, niko tayari kuongoza juhudi za kuwapatanisha Bw Gachagua na Bw Kenyatta. Sababu ni kuwa, si vizuri wakati eneo hili linagawanyika kisiasa, ilhali ndilo lenye idadi kubwa zaidi ya wapigakura nchini. Tutapata mafanikio kama eneo kupitia umoja wa kisiasa miongoni mwa viongozi wetu,” akasema.

Mwanaharakati huyo pia anashinikiza ukanda huo kuwa na chama kimoja cha kisiasa, ili kuboresha usemi wake kitaifa linapotetea maslahi yake.

Mwanaharakati David Kimengere wa chama cha Kuungana Kujenga Kenya: Sauti ya Mnyonye. PICHA | MAKTABA

Ili kutimiza hayo, amesajili chama chake—Kuungana Kujenga Kenya: Sauti ya Mnyonye—“ili kuwa jukwaa la ukanda huo kuendeleza sauti yake”.

“Kama eneo, tunahitaji chama chetu cha kisiasa, hasa wakati huu tunapopigania kutengewa raslimali kwa mfumo wa kura moja-shilingi moja-mtu mmoja. Uwepo wa chama cha kisiasa utahakikisha kuwa tunatoa sauti moja kama eneo, jambo litakalofufaa sana,” akasema.

Anaeleza wakati umefika wanaharakati wanaoonekana kutokuwa wenye ushawishi kuanza kusikilizwa na viongozi wa kisiasa, kwani hata wao wana maono na hoja nzito ambazo huenda zikaisaidia nchi katika siku za usoni.

“Viongozi wa kisiasa wanafaa kufahamu kuwa licha ya kutokuwa na ushawishi mkubwa, bado tunaweza kutoa michango muhimu kuhusu masuala tofauti yanayoiathiri nchi. Changamoto yangu kwao ni kuanza kumpa kila mtu nafasi kwani, kwa namna moja, hatungekuwa tukishuhudia migawanyiko ya kisiasa iliyopo Mlimani ikiwa kauli yangu ingezingatiwa hapo awali,” akasema.