Makala

Malakisi: Mji wa kale Magharibi mwa Kenya wajaribu kuamka usingizini

May 17th, 2024 5 min read

NA JESSE CHENGE

MJI wa Malakisi umekuwepo tangu mwaka 1848.

Malakisi ni mmojawapo wa miji ya kale zaidi Magharibi mwa Kenya na ulibahatika kuwa na viwanda vya kwanza katika eneo hilo.

Ukiwa umetulia baina ya kaunti za Bungoma na Busia, mji huu wa Malakisi wakati wa sifa zake, ulihudumia kwa uaminifu wakazi wa Sirisia, Bumula, na Teso Kaskazini kwa zaidi ya miongo mitatu.

Kipindi hicho, kilimo cha pamba kilikuwa na mafanikio makubwa katika mji huo.

Bidhaa kutokana na pamba Malakisi ziliuzwa kote Afrika Mashariki.

Malakisi inatokana na neno la Bukusu ‘Malikisi’ kumaanisha pahali pa dhahabu.

Ni mahali ambapo kitu kinaweza kuchimbwa. Ni mji wa pili wa kale zaidi magharibi mwa Kenya baada ya mji wa Mumias.

Ni mji uliovutia makabila yote nchini Kenya na Uganda vilevile.

Mji wa Malakisi ulikuwa sehemu ya historia ya ukuaji wa mji wa Chepkube, kwani wengi wa watu waliojihusisha na biashara ya usafirishaji haramu wa kahawa ambayo ilikuwa inafanikiwa katika mji wa mpakani wa Chepkube, walikuwa wafanyabiashara wenye ushawishi katika mji wa Malakisi.

Mkuu wa Chama cha Biashara cha Kenya National Chamber of Commerce (KNCC) eneo la Bungoma, Bw Haman Kasili aliambia Taifa Leo kwamba mji huo ulikuwa na uwezo mkubwa lakini biashara haramu ikaanza kuutia doa.

“Watu wengi waliokuwa wakifanya usafirishaji haramu wa kahawa walikuwa wakilala Malakisi na kwenda kununua kahawa Chepkube. Wamiliki wa hoteli katika mji wa Malakisi waliendesha biashara ya kahawa Chepkube,” alisema Bw Kasili.

Kihistoria, eneo la zamani la Malakisi chini ya ukoloni lilijumuisha sehemu za Teso Kaskazini, jimbo la Sirisia, wilaya ya Cheptais, maeneo ya Kabuchai n ahata Kimilili.

Mkuu wa kwanza wa enzi za ukoloni Malakisi katika miaka ya arobaini (1940s) alikuwa anaitwa Murunga Shiundu ambaye alitawala kutoka mji wa mpakani wa Malaba uliopo sasa, Kakapeli, Moding’, Lwakhakha, Cheptais katika mlima Elgon, Chwele hadi Kimilili.

Baada ya uhuru, kulikuwa na ugawanyaji wa huduma za serikali na uundaji wa mipaka mipya ambao ulisababisha kugawanyika na uundaji wa maeneo mapya kutoka eneo la zamani la Malakisi.

Kwa sasa, maeneo ya Bukokholo, Sitabicha, na Tamlega yanafanya sehemu ya wilaya ya Malakisi na makao makuu ya wilaya yako katika mji wa Malakisi.

Mto Malakisi ambao haukauki, unatiririka katika pembezoni mashariki mwa mji wa Malakisi kutoka Mlima Elgon.

Aidha milima ya Mwalie inatenganisha Teso Kaskazini katika Kaunti ya Busia na eneo la Sirisia katika Kaunti ya Bungoma.

Mji wa Malakisi unajivunia hospitali ya Malakisi ya kiwango cha Level 3 ambayo hutoa huduma za afya kwa mji mdogo na idadi ndogo ya wafanyakazi katika kampuni ya sigara ya British American Tobacco.

‘Mwiyala wa mango’ ni sehemu ambapo mwanaume wa kwanza wa Bukusu aliyeitwa Mango, alifanyiwa upashaji tohara baada ya kumuua nyoka mkubwa aliyemeza mbuzi ambao walikuwa ni mali ya ‘Barwa’ ambao wanafikiriwa kuwa Wamaasai waliokuwa wakiishi ndani ya Malakisi.

Mwaka 1948, Wabukusu walipinga majeshi ya Waingereza huko Malakisi.

Maasi hayo dhidi ya mkoloni yalisababisha mauaji ya mamia ya wafuasi wa Dini ya Musambwa. Elijah Mwasame Masinde, mwanzilishi wa Dini ya Msambwa, aliongoza uasi huo.

Elijah Masinde alitazamwa kama mkombozi wao dhidi ya ukoloni na harakati yake kama dini halali na ya kweli.

Bw Suleiman Sisungo, mkazi wa mji wa Malakisi, anasema Masinde alianza harakati hizo mwaka 1948 baada ya ‘kushauriana’ na nguvu fulani katika Mlima Zion (sasa Mlima Elgon).

Masinde aliwaambia wafuasi wake kwamba alikuwa amezungumza na Mungu ambaye alimwambia kuwa utawala wa watawala wa kikoloni ulikuwa umefikia mwisho na mwisho wa unyonyaji na matumizi mabaya ya kikoloni vilikuwa vimefika mwisho.

Masinde baadaye aliongoza jamii katika mapambano ya vurugu na Waingereza mwaka 1948.

Walianzisha uasi kama mapambano ya uhuru wa ibada huku wakiwatishia ‘watawala’ kifo kupitia barua.

Kikundi hicho kilishambulia na kuharibu mali za wakazi waliokataa kushirikiana nao na wale waliokuwa wakiwafadhili wakoloni katika kampeni za mkakati.

“Baadhi ya manusura ambao walikuwa wanaishi na risasi milini mwao waliokufa mwaka 2023 ni pamoja na marehemu Richard Nangaka, Samson Wamukekhe, na Kayo Lukorito,” aliongeza Bw Sisungo.

Malakisi ina kituo cha mafunzo ya usalama ambacho kimevamiwa na wakazi na kusababisha hatari kubwa baada ya serikali kuwaonya waondoke.

“Serikali inapaswa kuingilia kati na kurejesha ardhi kwa ajili ya kituo cha mafunzo ya usalama ambacho kinapaswa kubadilishwa kuwa chuo ili kuunda fursa za biashara kwa watu wanaoishi hapa,” aliongeza.

Kuanzia mwaka 1949 hadi 1966, biashara ya kilimo cha pamba ilifanikiwa na wakulima zaidi ya 21,000 walikuwa wakifurahia matunda ya jasho lao.

Fedha zilikuwa zinatiririka kwa wingi Malakisi, hasa baada ya kuanzishwa kwa kiwanda cha kusaga pamba nje kidogo ya mji.

“Malakisi ilikuwa mji mkuu wa viwanda wa Bungoma. Kiwanda hicho kilizalisha sabuni ya Udo, mafuta ya kupikia ya Udo, chakula cha mifugo, na pamba, miongoni mwa bidhaa nyingine,” anakumbuka Bw Mohamed Lukhale.

Mji ulifanya kazi kama mashine iliyopangwa vizuri ambapo wakulima walipokea malipo kwa wakati kwa mazao yao ya pamba, na wafanyakazi wa kiwanda walipokea mishahara yao kila mwezi bila kukosekana.

Katika miaka ya themanini (1980s), Jiwas Bakery iliongeza hadhi ya kibiashara ya eneo hilo. Mkate ulisambazwa kote magharibi mwa Kenya, Kisumu, Pokot Magharini na hata nchi jirani ya Uganda.

Wawekezaji walimiminika katika mji huo, na kampuni za Mastermind Tobacco na British American Tobacco (BAT) ziliweka maduka.

Walimwaga mamilioni ya pesa katika viwanda na kuajiri wakulima waliopata bidi ya kupanda tumbaku. Mji huo baadaye ulipandishwa hadhi kuwa baraza la mji lenye kata tano ambazo ni Sitabicha, Tamulega, Mwalie, Siboti/Netima, na Napara. Walakini, kadri miaka ilivyosonga mbele, matatizo yalianza kujitokeza.

Kuporomoka kwa mji wa Malakisi kumetajwa kuwa ni matokeo ya sababu kama vile usalama hafifu, kuingiliwa kisiasa, na sera mbaya za serikali. Ukuaji wa haraka wa mji huo zama zile ulivutia nguvu chanya na hasi ambazo hatimaye zilisababisha kuanguka kwake.

“Malakisi ilianza kufifia kutokana na usalama kudorora, kuingiliwa kisiasa, na sera za serikali za kutoza ushuru mzito kwa wawekezaji zilizowafanya wafunge viwanda vyao na kuingia katika biashara nyingine mahali pengine,” akasema Bw Kasili.

Mwaka 1996, wakulima walipata mali za kiwanda cha kusaga pamba, lakini kiwanda hicho kilianguka na kusitisha shughuli zake mapema miaka ya 2000.

Kufikia mwaka 2005, wachuuzi wa vyuma chakavu waliharibu vifaa katika kiwanda hicho.

Maduka mengi yalifunga mjini Makakisi. PICHA | JESSE CHENGE

Leo, mji wa Malakisi ambao zamani ulikuwa na shughuli nyingi sasa umebaki kuwa gofu, na majengo yaliyotelekezwa na alama za hasara zinazoweza kuhisiwa na kuonekana.

“Leo hii, sauti ya kufurahisha ya kiwanda cha kusaga pamba imechukuliwa na sauti ya kelele za mijusi,” anasikitika Willy Opili, mwenyekiti wa Cooperative Cotton Ginnery Malakisi.

“Tulibaki bila kitu. Baadhi ya mashine ziliibiwa. Watu wengi walipoteza kazi zao,” akaongeza.

Wafanyabiashara wengi ambao walifungua maduka katika mji wa mpakani walihamisha biashara zao kwenda Bungoma, Malaba, Kimilili, Kitale, Eldoret na Nairobi.

Katika miji hiyo, ambayo zamani ilikuwa vituo vya biashara na viwanda vilivyofanikiwa, sasa imegeuzwa kuwa makumbusho ya kivuli cha zamani.

Bw Sisungo aliomba viongozi wa kisiasa kuacha tabia ya kutoa zawadi na badala yake kuweka mashirika ambayo yanaweza kufufua uchumi wa mji.

“Wanaweza kuanzisha kambi ya chuo kikuu, kituo cha mafunzo ya matibabu, au shughuli za kibiashara. Kuweka lami kwenye barabara ya Kimaeti-Lwakhakha ambayo ni njia fupi kwenda Sudan kutafufua Malakisi kwani madereva wa malori wataweza kupumzika na kulala hapa,” alisema Bw Sisungo.

Wazo la kurudisha kilimo cha pamba linaweza lisiwezekane, kwani kwa sasa ardhi imegawanyika na kupanda pamba kwenye nusu ekari haifai kiuchumi.

Pamba inahitaji maeneo makubwa ya ardhi wakati sehemu kubwa ya ardhi imeuzwa kulipa ada za shule baada ya kushuka kwa viwanda vya ndani. Serikali inaweza kuchochea ukuzaji wa njugu, alizeti, mtama, ulezi, macadamia, mafuta ya mzeituni, mbegu za Benne au sesame, mbegu za Castor, Canola, karanga za Bambara, jojoba, mbegu za kitani na ufuta ili kuzalisha mafuta ya kula.

“Hadi sasa, BAT, Mastermind, taasisi za kifedha, na kiwanda cha kusaga pamba vimefunga biashara zao. Kilichobaki katika mji wa Malakisi ni hisia ya huzuni,” akasema.

Kushuka kwa miji hii kunatukumbusha kwa nguvu umuhimu wa maendeleo endelevu na umuhimu wa utawala bora ili kuzuia kuachwa kwa jamii zilizokuwa hai hapo awali.

Hii ni wito wa viongozi kuchukua hatua na kushughulikia masuala ambayo yamesababisha kuanguka kwa miji hii na kufanya kazi ya kufufua miji hiyo kwa faida ya wanajamii na taifa kwa ujumla.