Waititu: Mlima Kenya kutoa mgombea urais 2027
NA MWANGI MUIRURI
ALIYEKUWA Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu amesema haoni faida ya watu wa Mlima Kenya kuunga mkono mtu kutoka nje ya eneo hilo kuwania urais.
Akihutubu Ijumaa katika Kongamano la Limuru III, Bw Waititu alisema “ni lazima sisi na kura zetu zote tuwe tukisimama na mtu wetu hadi kwa debe”.
“Mimi ninawaomba msamaha kwa kuwa nilikuwa mmojawapo wa waliotumika kumvumisha mgombea wa urais kupitia muungano wa Kenya Kwanza ambao serikali yake kwa maoni yangu imegeuka kuwa dhalimu,” akadai Bw Waititu.
Bw Waititu ambaye alishtakiwa kwa kudaiwa kutekeleza kashfa ya wizi wa Sh588 milioni alipokuwa Gavana wa Kiambu, alisema kura 8 milioni sio za kujazia wengine chache zao ndio watawale.
Bw Waititu alisema kwamba tayari amejiondoa kutoka chama cha Rais William Ruto cha United Democratic Alliance (UDA) na hatimaye kujiunga na vuguvugu la raia wa kawaida, yaani ‘Wanjiku Mashinani’.
Bw Waititu alisema kwamba hata wadhifa wa Gavana wa Nairobi unafaa kushikiliwa na mtu kutoka Mlima Kenya.
“Wadhifa wa Gavana wa Nairobi ni wa maana sana kwa watu wa Mlima Kenya kwa kuwa ndio husimamia mamlaka ya serikali ya kaunti hiyo ambayo ni kitovu cha biashara,” akasema.
Pia aliongeza kwamba harakati za kutafuta mwaniaji wa urais ifikapo 2027 zimeanza.