Habari za Kitaifa

Mawaziri matatani kwa kufurusha wakazi wa mitaa ya mabanda

May 17th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA RICHARD MUNGUTI

MAWAZIRI watatu wameshtakiwa na Shirika la Kutetea Haki za Binadamu nchini (KHRC) kwa kuwatimua wakazi wa mitaa ya mabanda ya Mukuru kwa Njenga, Mukuru kwa Reuben, Mathare na kijiji cha Mai Mahiu bila ya kuwapa makao.

KHRC inaiomba Mahakama Kuu iwashurutishe mawaziri wa Usalama wa Ndani Prof Kithure Kindiki, Waziri wa Mazingira na Misitu Bi Soipan Tuya na Waziri wa Ardhi na Nyumba Bi Alice Wahome kuwapa makazi mapya waathiriwa hao wa mafuriko ambayo yamesababisha watu takriban 300 kuaga dunia.

Endapo wananchi wataendelea kufurushwa makwao bila ya kupewa makazi na huduma nyingine, basi KHRC imeomba mahakama utimuaji wakazi wa maeneo yanayodaiwa kuwa hatari kwa usalama wa wananchi ukomeshwe hadi pale serikali itakapopata pahala pa kuwahamishia.

Mvua ya gharika ilishuhudiwa katika maeneo mengi nchini.

KHRC imeeleza mahakama kwamba janga hili la mafuriko limesababisha watu zaidi ya 600,000 kuachwa bila makazi na shule za umma zimegeuzwa kuwa makazi yao ya muda.

Mahakama imeambiwa mawaziri hawa walilala kazini kwa vile Idara ya Hali ya Hewa ilitangaza 2023 kwamba mvua ya El Nino ingenyesha na tena Februari 2024 pia idara hiyo ilitangaza kwamba mvua kubwa ingenyesha na serikali ikanyamaza kimya.

Mawakili Kelly Malenya na Haggai Chimei walifichua katika kesi waliyomshtaki Prof Kindiki kwamba aliamuru watu wanaoishi karibu na mito na mabwawa wafurushwe bila ya kuwapa makazi.

Mahakama ilielezwa kwamba agizo hilo la waziri huyo wa usalama wa ndani limekandamiza haki za wahanga wote ambao sasa wanaishi katika mahema bila chakula na huduma maalum.

Mawakili hao walisema kwamba agizo la Prof Kindiki kwamba watu wanaoishi mita 30 kutoka mitoni wafukuzwe kabisa halina mashiko kisheria kwa vile alistahili kutenga pahala ambapo wangepelekwa kisha aamuru waondoke.

“Mvua kubwa iliyonyesha maeneo mengi nchini ilisababisha maelfu na maelfu ya watu kuathirika. Mamia ya watu wamekufa na mali nyingi kuharibiwa ikiwa ni pamoja na mazao ya vyakula,” mawakili Malenya na  Chimei walisema katika kesi waliyowasilisha kortini.

Mbali na mawaziri hao watatu, Mamlaka ya Maji Nchini (WRA), Mamlaka ya Uhifadhi wa Mazingira Nchini (Nema), Baraza la Magavana nchini (CoG), Mamlaka ya Kupambana na Majanga (NDMA), Shirika la Reli Nchini (KRC) na Mwanasheria Mkuu (AG) pia wameshtakiwa na KHRC.

Mahakama iliombwa iamuru mamlaka ya maji iwasilishe mahakamani ripoti kuhusu mabwawa yote nchini na usalama wa watu wanaoishi katika maeneo yaliyo karibu.