Habari za Kaunti

Ubomoaji: Familia 1,000 zapoteza makao South B

May 17th, 2024 2 min read

NA SAMMY KIMATU

ZAIDI ya familia 1,000 katika mitaa miwili ya mabanda katika tarafa ya South B, Kaunti ndogo ya Starehe wanakesha nje kwenye baridi kali baada ya serikali kubomoa makazi yao kufikia Alhamisi jioni.

Akiongea na wanahabari wakati wa shughuli hiyo, Naibu Kamishna wa Kaunti-ndogo ya Starehe, Bw John Kisang, alisema hilo lilifanyika kwa kutii agizo la Rais William Ruto kwamba watu wote wanaoishi katika kingo za mito na maeneo ya mikondo ya maji waondoke au wafurushe kwa lazima.

Aidha, Bw Kisang alieleza kwamba watu hao ni wakazi kutoka mtaa wa mabanda wa Mukuru-Shimo La Tewa na wenzao kutoka mtaa wa mabanda wa Mukuru-Mariguini.

“Familia 860 zimeathirika katika mtaa wa Mariguini hali zaidi ya familia 300 kutoka mtaa wa Mariguini waliondoka kwenda kwingineko. Hata hivyo, waliondoka kwa hiari yao bila kulazimishwa au kudhulumiwa. Walikuwa na fursa pia ya kukusanya, kupanga na kuondoa mali yao,” Bw Kisang akasema.

Vilevile, Bw Kisang alieleza kwamba nyumba za walioondoka zilikuwa katika kingo za Mto Ngong huku zikiwa katika eneo lililopimwa na serikali la kuwa katika umbali wa kuanzia mita 30 kutoka kwenye Mto Ngong.

“Serikali ilitoa maagizo na amri ya kufuata kwamba watu wawe umbali wa angaa mita 30 kutoka kwenye ukingo wa mto, sio tu katika Kaunti ya Nairobi bali katika kila pembe ya nchi ili kuepusha athari za mafuriko kutokana na mvua nyingi inayoendelea kunyesha kote nchini na kuleta maafa,” akasema.

Wakati wa shughuli hiyo, tingatinga la wanajeshi ndilo lililohusika katika ubomoaji wa nyumba, mabanda na majengo yote ‘yasiyotakikana’.

Shughuli ya ubomoaji ikiendelea South B. PICHA | SAMMY KIMATU

Mkuu wa polisi Makadara, Bi Judith Nyongesa, aliambia Taifa Leo kwamba maafisa wa polisi wa kupambana na ghasia (GSU) wametumwa kuweka usalama katika maeneo yaliyolengwa.

“Nina maafisa wa kutosha niliotuma kudumisha usalama katika maeneo yote yanayobomolewa. Katika mtaa wa Shimo La Tewa, kundi la vijana lililokuwa likijipanga kupora mali ya wananchi lilikuwa na wakati mgumu kutumia fursa ya kuvuna wasikopanda baada ya kufurushwa na polisi,” Bi Nyongesa akasema.

Kadhalika, aliongeza katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Mariguini, kundi jingine la vijana lilitupia maafisa wa polisi mawe kwa lengo la kupata mwanya wa kukata vyuma kutoka kwa majengo yaliyobomolewa.

“Polisi walilazimika kufyatua mikebe ya vitoa machozi ndiposa vijana hao wakatoroka na utulivu ukarejea na ubomoaji ukaendelea,” akasema.

Watu wanaoishi karibu sana na kingo za maji waagizwa kuhama. PICHA | SAMMY KIMATU