Makala

Mjukuu wa sodo: Mama asimulia alivyoitwa nyanya bintiye alipokosa taulo za hedhi 

May 18th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA FRIDAH OKACHI

UKOSEFU wa taulo za hedhi maarufu kama sodo ni mojawapo ya changamoto zinazokumba wanawake nchini, haswa wanaotoka katika familia zenye mapato ya chini.

Mahangaiko hayo yanakuwa kama kutia chumvi kwenye kidonda kinachouguza kwa wenyeji wa mitaa ya mabanda.

Virginia Muthoni Murimi ni mkazi wa mtaa wa mabanda wa Kabiria, eneo la Riruta, Dagoretti Kusini, Kaunti ya Nairobi na anakumbuka alivyoitwa nyanya kwa sababu ya bintiye kukosa sodo.

Kwenye mahojiano ya kipekee Ijumaa, Mei 17, 2024 na Taifa Dijitali, baada ya kushiriki kikao cha wabunge wanachama wa kamati ya Bajeti Bungeni kukusanya maoni ya umma kuhusu Makadirio ya Bajeti Mwaka wa Fedha 2024|2025, Muthoni ambaye ni mama wa wasichana sita, alisema kifungua mimba wake alipachikwa mimba kwa sababu ya kukosa taulo za hedhi.

“Alikuwa na rafikiye wa kiume ambaye kumbe nia yake haikuwa njema, na hatimaye aliishia kupata ujauzito kwa ahadi ya kumnunulia taulo za hedhi. Hivyo ndivyo niliishia kuitwa nyanya, nina mjukuu wa sodo,” aliambia Taifa Dijitali.

Bintiye alikuwa kidato cha pili.

Wakati wa mahojiano, Muthoni, 49, alishangaza akisimulia jinsi wanawe hutumia sodo zilizotumika.

“Nyakati zingine, wasichana wawili hulazimika kutumia sodo moja kwa awamu,” alielezea.

Wakazi wa Dagoretti Kusini na Kaskazini wakati wa mkutano wa Umma katika Ukumbi wa BP Empowerment Centre, Nairobi kwenye kikao cha umma na wabunge wanachama wa Kamati ya Bajeti Bungeni. PICHA| FRIDAH OKACHI

Hali hiyo inachangiwa na ufukara unaomkumba, ikizingatiwa kuwa hufanya vibarua (kazi ya nyumba) akikadiria kuingiza Sh150 kwa siku.

Hesabu, kufuatia dokezi zake inaashiria kuwa kwa mwezi – akifanya kazi siku 30, huingiza pato la Sh4, 500.

Amekodi nyumba Nairobi, na wanawe wanamtegemea kwa mahitaji muhimu ya kimsingi, ikiwemo chakula, mavazi na karo.

Huku gharama ya maisha ikiendelea kupanda kila uchao, wanawe wawili wamelazimika kuacha shule kwa sababu ya umaskini.

Kwenye kikao cha wabunge na umma kuelezea maoni yao kuhusu Makadirio ya Bajeti 2024|2025, Muthoni alishangaza kamati ya Bajeti Bungeni jinsi anang’ang’ana kusukuma gurudumu la maisha Nairobi.

“Nina wasichana sita na kila mmoja anahitaji sodo. Pakiti ya taulo sita za hedhi za hedhi inauzwa Sh65, juu kutoka Sh50. Ni watoto nitanunulia chakula au ni sodo?” akataka kujua.

Mchakato huo wa umma na wabunge kuhusu bajeti inayotarajiwa kusomwa Juni 2024, ulihudhuriwa na mchakato wa Kutengeneza bajeti uliohudhuriwa na Mbunge wa Dagoretti Kusini, John Kiarie almaarufu KJ, Mbunge Mwakilishi wa Kike Nairobi, Bi Esther Passaris, na Mbunge wa Embakasi Mashariki, Babu Owino.

Bi Passaris aliahidi kuwa atasaidia kushinikiza viongozi wengine wa kike kuhakikisha matatizo ya sodo yanatatuliwa ipasavyo.

“Kumekuwa na usambazaji wa sodo lakini ninajua sio kila msichana anapata. Tutasukuma serikali ipunguze bei ya bidhaa hiyo muhimu kwa wanawake,” Bi Passaris alisema.