Habari za Kitaifa

Ahadi ya polisi kuongezwa mishahara huenda ikageuka ‘hewa’

May 19th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA CHARLES WASONGA

NDOTO ya maafisa wa polisi ya kupata nyongeza ya mishahara ya angalau asilimia 40 mwaka huu 2024 huenda ikakosa kutimia baada ya Wizara ya Fedha kufeli kutenga Sh15 bilioni za kutekeleza nyongeza hiyo katika Makadirio ya Bajeti ya mwaka ujao wa kifedha wa 2024/2025.

Akipokea ripoti ya jopokazi la kuchunguza viwango vya mishahara ya maafisa hao na mazingira yao ya kikazi mnamo Novemba 28, 2023, Rais William Ruto aliahidi kuwa serikali ingetekeleza mapendekezo yake yote, ikiwemo nyongeza ya mishahara ya polisi na maafisa wa magereza.

Jopokazi hili lililoongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu David Maraga ndilo lilipendekeza kwamba polisi, maafisa wa magereza na wale wa Shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) waongezwe mishahara kwa angalau asilimia 40.

Akiongea katika Ikulu ya Nairobi alipopokea ripoti hiyo, Dkt Ruto alipongeza mapendekezo yake akisema yatarejesha maadili, ufanisi na uwajibikaji katika vikosi hivyo vya usalama.

“Lengo letu la kimsingi ni kufanikisha mabadiliko nchini kwa hakikisha kuwa sekta ya usalama inaendesha majukumu yake kwa viwango vya juu vya utaalamu, uadilifu na uwajibikaji. Na hii itawezekana kupitia kuimarishwa kwa masilahi na kuboreshwa kwa mazingira ya utendakazi wa maafisa hao,” Dkt Ruto akakariri.

Naibu Rais Rigathi Gachagua pia amekuwa akikariri ahadi hiyo akisema hatua hiyo itawatia moyo polisi wanapotekeleza wajibu wao wa kulinda mali na maisha ya Wakenya.

Lakini kulingana na stakabadhi zilizowasilishwa mbele ya Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Usalama na Inspekta Jenerali wa Polisi Japhet Koome mnamo Ijumaa, Sh15 bilioni zilizonuiwa kutumika kutekeleza nyongeza hiyo kwa maafisa wa asasi hiyo ya Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) hazikuwekwa katika mgao wa bajeti katika mwaka wa kifedha wa 2024/2025.

“Nawaomba enyi wabunge kuamuru kurejeshwa kwa pesa hizo, ambazo ni sehemu ya Sh60.61 bilioni ambazo ziliondolewa kutoka kwa mgao wa bajeti ambao NPS iliomba,” Bw Koome akaiambia Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Narok Magharibi Gabriel Tongoyo katika Ukumbi wa County, majengo ya Bunge.

Inspekta Jenerali huyo wa polisi alisema jopo la Bw Maraga lilipendekeza kuwa nyongeza hiyo ya mishahara kwa polisi itekelezwe kwa awamu tatu kuanzia mwaka wa kifedha wa 2024/2025, hadi ule wa 2026/2027.