Akili Mali

Sasa kuna teknolojia ya kukwambia unavyoweza kutumia ardhi kwa manufaa zaidi

April 3rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA RICHARD MAOSI

Ardhi ni zana muhimu kwa ajili ya kutosheleza mahitaji ya chakula nchini.

Wataalam wanasema mbali na kuwa utajiri, matumizi yake yanastahili kuongeza thamani kwa maisha ya wakulima au wafugaji.

Kwa upande mwingine umiliki wa ardhi umebadilisha mtazamo wa maisha ya wakulima wadogo mashinani na hivyo basi kuimarisha kiwango cha uzalishaji wa chakula na kuinua kiuchumi.

Mike Mudenyo ambaye ni afisa Mratibu wa Miundo mbinu (physical planner) kutoka Kaunti ya Laikipia anasema hii ni mojawapo ya Kaunti nchini ambazo zimepiga hatua na wameanzisha maabara maalum ya kutathmini ukubwa wa ardhi na matumizi yake.

Maabara yenyewe inatumika sio tu kwa kutoa taarifa na kuunganisha kila eneo la ardhi bali pia kuwasaidia wafugaji waweze kufikiwa na huduma za serikali.

Akilimali ilizuru Kaunti ya Laikipia ambapo tulikumbana na jamii ya wafugaji ambao wanaungama kwamba teknolojia imerahisisha mambo, karne hii ya 21, ambayo umiliki wa ardhi umezingirwa na changamoto.

Kwa ushirikiano na serikali ya Kaunti ya Laikipia , wakazi wa Musul ambao ni zaidi ya 700 wamemudu kufaidika na programu ya uendeshaji shughuli ya kumiliki ardhi kidijitali.

“Asilimia 68 ya wakenya hawana stakabadhi sahihi za kuonyesha umiliki wa ardhi,” anasema Husna Mbarak. Bi Husna Mbarak ni meneja wa Programu za Usimamizi wa Ardhi kutoka shirika la Lishe la Umoja wa Mataifa FAO.

Anasema umiliki wa ardhi kidijitali utawasaidia wakulima kufahamu kiwango cha rasilmali ambazo wanamiliki.

Aidha, kutawasaidia wakulima kupata taarifa kuhusu uwepo wa rasilmali za asilia kama vile viumbe wa majini, misitu, chemchemi na maeneo kame.

“Maana yake wanaweza kuwekeza ipasavyo kwa ajili ya manufaa ya wakazi kama kitega uchumi na kwa wakati huohuo kuyatunza mazingira,” asema.

Tatu, umiliki wa ardhi kidijitali umewasaidia wakazi wa sehemu hii ya Laikipia kugawanya shamba vipande mbalimbali kwa ajili ya matumizi tofauti kama vile sehemu maalum ya mifugo, mimea na sehemu ya mkulima kuishi.

Isitoshe, Husna aliambia Taifa Leo kwamba ni utaratibu ambao kwa asilimia kubwa umewezesha wafugaji wa kuhamahama hususan katika maeneo kame kupunguza visa vya kupigania malighafi mara kwa mara.

Pia watakuja na njia mbadala ya kusuluhisha matatizo yao.

Maeneo kame kama vile Samburu, Isiolo, Marsabit na sehemu kubwa za Laikipia ni makazi rasmi ya wafugaji wa kuhamahama lengo kuu likiwa ni kusaka malisho na maji.

Ili kupunguza shinikizo katika ardhi yao baadhi ya wafugaji siku hizi hasa akinamama wameanza kuendesha kilimo cha mboga, na matunda.

Kwa upande mwingine Husna anasema mabadiliko ya tabia nchi na shughuli za kibinadamu katika mazingira zimekuja na athari hasi katika mazingira. ambazo hufanya ardhi kuwa jangwa.

Hii ndio sababu Shirila la Umoja wa Kimataifa limeanzisha mikakati kwa Ushirikiano na Muungano wa Mataifa ya Ulaya (EU) pamoja na serikali za ugatuzi wanafadhili miradi wa kusajili ardhi kidijitali.

Miradi wenyewe inalenga Kaunti 47 za Kenya hii ikiwa ni awamu ya pili.

Anasema ushirikiano huu ni muhimu kwa sababu huleta suluhu la kudumu kudhibiti visa vya kugombania mali asilia.

Kwa upande mwingine, migogoro kati ya wakulima na wafugaji inaweza kutatuliwa kwa urahisi na kuwekwa mipango maalum ya matumizi ya ardhi.

Eneo la Musul viungani mwa Kaunti ya Laikipia ni miongoni mwa maeneo ya wafugaji ambayo yamefaidi mradi wenyewe ambapo kufikia sasa wanamiliki zaidi ya ekari 2,600 kama jamii almaarufu Community Land.