Bei ya Omena yapanda maradufu kutokana na gharama ya maisha
BEI ya samaki aina ya dagaa almaarufu Omena, imepanda maradufu kutokana na kuongezeka kwa gharama ya maisha na mvua kubwa inayonyesha.
Uchunguzi wa Taifa Leo umebaini kuwa, katika kaunti ya Siaya, familia nyingi hazinunui Omena kwa kutomudu bei masokoni.
“Kupikia familia yangu ugali kwa sukuma wiki na omena kila siku ni vigumu. Ninaweza kuwa na ugali na sukuma wiki bila omena au kuwa na Sikuma wiki na Ugali,” Bw Joash Owino, mhudumu wa bodaboda katika mji wa Siaya na baba wa watoto watatu alisema.
Bw Owino anaeleza kuwa licha ya uhaba wake, bei ya Omena imekuwa ikipanda mara kwa mara.
“Leo unanunua mkebe wa gramu 250 kwa Sh70, kesho yake bei itapanda hadi Sh100. Bei inaamuliwa na mambo mengi kama vile bei ya mafuta, sheria katika maeneo ya kuvua samaki katika Ziwa Victoria na kutegemea misimu ya mwaka,” alieleza.
Katika kaunti tano zinazopakana na Ziwa Victoria ambapo samaki hao wanapatikana, bei ya mkebe wa kilo 2 almaarufu gorogoro ni kati ya Sh400 na Sh500.