Miguu yangu imefura na kujaa majipu ila daktari haoni tatizo!
Mpendwa daktari,
MIGUU yangu imefura kwa miezi kadhaa sasa, na pia sehemu hii imejaa majipu na hivyo kunisababishia maumivu mengi. Nimeenda katika hospitali kadhaa na kila mara madaktari wanasema kwamba hawaoni tatizo. Shida yaweza kuwa gani?
Hadijah, Mombasa
Mpendwa Hadijah,
Kukiwa na mkusanyiko wa majimaji chini ya ngozi au katikati ya tishu, hali hii inafahamika kama oedema.
Hali hii yaweza kukumba miguu, sehemu inayozunguka kifundo cha mikono na miguu au hata katika sehemu nyingine za mwili kama vile sehemu inayozingira ubongo, moyo, mapafu na kwenye tumbo.
Hali hii yaweza kuwa mbaya kiasi cha kusambaa kwa kasi na kurejea hali ya kawaida baada ya kipindi kifupi. Hii yaweza kusababishwa na kuteguka, maambukizi, mgando wa damu, mng’ato wa nyuki au nyigu, mzio, na matatizo ya figo au moyo.
Yaweza pia kuwa mbaya zaidi na kuzorota muda unavyozidi kusonga. Hali hii yaweza kutokana na matatizo ya mzunguko wa damu, au mtiririko wa maji maji ya limfu, matatizo ya moyo, figo, ini, maradhi ya kikoromeo, kiwango cha chini cha damu au uvimbe kwenye fupanyonga.
Unapaswa kufanyiwa uchunguzi wa kina ikiwa ni pamoja na kuangalia iwapo kuna maambukizi, maradhi ya ini, figo, kikoromeo, matatizo ya moyo. Picha itapigwa kuchunguza mtiririko wa damu katika sehemu ya chini ya mguu, tumbo na fupanyonga.
Njia bora ya kutibu oedema ni kwa kukabiliana na tatizo lililopo. Ikiwa oedema inatokana na matatizo ya mzunguko wa damu, utafaidi kutokana na stokingi maalum za kubana zinazofahamika kama compression stockings, kuinua miguu na kufanya mazoezi ya miguu.