Serikali yaambia Uhuru: Tumia ile afisi ya Kibaki lau sivyo usahau kulipiwa kodi
MVUTANO unatokota baina ya serikali ya Rais William Ruto na aliyekuwa kiongozi wa taifa Uhuru Kenyatta kuhusu chaguo la afisi ya rais huyo mstaafu huku serikali ikianza kutekeleza kikamilifu Sheria kuhusu Marupurupu ya Marais Waliostaafu 2003.
Sheria hiyo inasema rais mstaafu aliye hai apatiwe afisi na wafanyakazi wa kudumu, watakaokuwa watumishi wa umma wanaolipwa kwa misingi ya Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC), marupurupu ya kustaafu, bima miongoni mwa mengine baada ya miaka ya kuhudumia taifa.
Serikali inamtaka Bw Kenyatta, ambaye ni Rais wa nne wa nchi, kutumia afisi iliyokuwa ya mtangulizi wake Mwai Kibaki kabla ya kifo chake mnamo Aprili, 2022, katika eneo la Nyari, Gigiri, jijini Nairobi.
Serikali inahoji kuwa makazi hayo ya Gigiri hayajakuwa yakitumika kufuatia kifo cha hayati Kibaki, rais wa tatu wa taifa.
Aidha, serikali inahoji kwamba itakuwa sawa na kufuja pesa za umma ikiwa afisi nyingine itasakwa kulipiwa kodi huku afisi ya Gigiri ikibaki tupu.
Duru za kuaminika serikalini zilizochelea kutajwa, zilieleza Taifa Jumapili kuwa rais mstaafu anapendelea makazi yake ya Caledonia, yaliyopo kando na ikulu, kama makazi yake ya kustaafu.
Iwapo chaguo la rais mstaafu litakubalika, itamaanisha kuwa serikali itamlipia kodi kwa mali yake binafsi.
Malipo ya marupurupu yaliyoidhinishwa kisheria kwa rais waliostaafu na manaibu rais, yameorodheshwa chini ya bajeti ya Masuala kuhusu Ikulu na Msimamizi wa Ikulu, ikiwemo mhasibu wa bajeti ya Ikulu kama mtekelezaji.
Aliyekuwa Mbunge wa Kajiado Kusini, Bw Katoo ole Metito, ndiye Misimamizi wa Ikulu kwa sasa na hakujibu maswali yetu.
Hata hivyo, afisa wa Ikulu ambaye hakutaka kutajwa, alisema japo rais mstaafu anataka kulipiwa kodi kwa nyumba yake mwenyewe, serikali haiko tayari kufanya hivyo.