Habari za Kitaifa

Mnataka nijiuzulu? Mtasubiri sana, Nakhumicha aambia wakosoaji

April 6th, 2024 1 min read

NA SHABAN MAKOKHA

WAZIRI wa Afya, Susan Nakhumicha, amewahakikishia Wakenya kwamba mazungumzo baina ya serikali na wahudumu wa afya wanaogoma yanaendelea vizuri, ili kumaliza mgogoro ulio katika sekta ya afya.

Waziri alisema hayo huku akiwahakikishia Wakenya kwamba anawafanyia kazi, na hatajiuzulu, kama vile ambavyo amekuwa akishinikizwa na baadhi ya viongozi.

Alisema ataendelea kuwatumikia Wakenya, kwani ameiweka Wizara ya Afya katika mwelekeo unaofaa.

“Tayari, tuna sheria mpya za kuidhibiti sekta hii. Nalichukulia suala hili la mgomo wa wafanyakazi kama nafasi nzuri kwetu kutathmini mwelekeo tulio nao; na ikiwa kuna mahali tunafaa kufanya marekebisho. Niko kazini, ninafanya kazi na nitaendelea kuwafanyia kazi Wakenya chini ya serikali ya Kenya Kwanza,” akasema Bi Nakhumicha.

Aliwarai viongozi wa wahudumu hao kuisaidia serikali kutafuta suluhisho la kudumu kwa migomo ambayo imekuwa ikishuhudiwa miongoni mwao kila mara.

Madaktari na wahudumu wengine katika sekta ya afya wamekuwa kwenye mgomo ambao umedumu kwa zaidi ya wiki tatu sasa wakipigania nyongeza ya mshahara na marupurupu.