Makala

Wahudumu wa biashara ya ngono Mlima Kenya wakosoa Gachagua kwa kufunga baa  

April 8th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MWANGI MUIRURI 

WAHUDUMU wa biashara ya mahaba kutoka Mlima Kenya wikendi walimkosoa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua, wakimtaja kama kama adui wa mahasla.

Wakiongea Mjini Karatina, Kaunti ya Nyeri Mjini, walisema sera nyingi ambazo Bw Gachagua anasukuma eneo la Kati ni za kuleta umaskini.

Karatina, kwa mfano, ambako ndiko nyumbani kwa Naibu wa Rais hakuna hata baa moja imebasalia ikihudumu, hivyo basi kuzidisha kilio.
“Ukifunga baa moja kama unavyofanya Bw Gachagua, jua tu umetimua wafanyakazi wa moja kwa moja wasiopungua watano huku wengine zaidi ya 50 wakipoteza mwanya wa kuchuuza bidhaa au wasanii kuburudisha,” akasema mshirikishi wao wa ukanda huo Christine Wambui.

Bi Wambui aliongeza kwamba ndani ya baa sio kunakotengenezewa pombe za mauti na sio kunakouziwa mihadarati.

“Huwezi ukasema unafunga mabaa kwa kiwango ambacho tunashuhudia eneo la Mlima Kenya katika harakati hizo ukiwapokonya kazi mamia ya mahasla na iwe wewe ni kipenzi cha wanyonge. Kufunga baa hakutazuia wa kutumia pombe aitafute iliko,” akasema.
Wahudumu hao wa biashara ya ngono walisema sera za Bw Gachagua eneo hilo zinachangia ongezeko la uhalifu na uasherati.
“Umaskini ukianza kupenya jamii, ukora huamka. Sisi ni makahaba wa kujiamlia, lakini umaskini sasa unashinikiza wengine ambao hata wako kwa ndoa kuanza kujiuza kimwili,” akasema.
Aliteta kwamba kwa sasa mashinani kumejaa mahangaiko kwa kuwa hata sekta za kilimo ambazo Bw Gachagua alikuwa ameahidi kufufua ili mapato yaimarike, bado ziko katika hali mahututi.
“Aidha, wataalamu wa kiafya watakwambia kwamba madhara ya kutamatisha ghafla uzoefu wa pombe na mihadarati huambatana na kusombwa na msongo wa mawazo, hasira zisizoeleweka na pia kutetemeka. Bw Gachagua hakuweka mikakati ya kukabiliana na hali hizo,” akasema.
Hata hivyo, Bw Gachagua amekuwa akishikilia kwamba vita hivyo havitalegezwa kwa vyovyote vile na yuko tayari kupoteza umaarufu wake katika vita hivyo.
“Mimi sijali kupoteza umaarufu wa kisiasa. Nani angetaka kuwa kiongozi wa walevi? Walevi na wauzaji pombe hawana ushawishi wa kisiasa na idadi yao haina maana katika uchaguzi,” akasema Bw Gachagua mnamo Februari 10, 2024 alipotembea Kaunti ya Murang’a.