Habari za Kitaifa

Wanawake Kenya wanavyogeuzwa tasa hospitalini bila idhini yao – Utafiti

April 9th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA LEON LIDIGU

WANAWAKE nchini wanaosaka huduma za matibabu ya uzazi wanafanyiwa ukaguzi wa sehemu za siri, kukatizwa uwezo wa kupata mimba na kufanyiwa upasuaji usiohitajika wanapojifungua bila idhini yao, ripoti mpya imebaini.

Pia wanalazimishwa kukubali matibabu au huduma za afya ambazo hawahitaji.

Hii ni kulingana na ripoti iliyotayarishwa na Chama cha Watu wanaoishi na Ulemavu Nchini (APDK), Shirika la Kuangazia Haki za Vijana-Kenya (CAARY-AFRICA), Nguvu Collective na washirika wengine.

Matokeo hayo yanafichua jinsi wahudumu wa afya katika kaunti 27 nchini Kenya hutoa huduma bila kuzingatia utu na heshima.

“Asilimia 68 ya visa hivyo vinakiuka haki za kibinadamu na ni vitendo vinavyowanyima wanawake haki zao za kutendewa utu na kupata huduma bora za afya wakati wa uja uzito, wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua,” waandishi wa ripoti hiyo wanasema kwa kurejelea data zilizotokana na matokeo ya utafiti wao

Ripoti hiyo inasema kuwa asilimia 94 ya wanawake katika kaunti hizo hawakuripoti visa vya kutendewa dhuluma hizo kwa sababu hawakujua namna ya kufanya hivyo.

Aidha, ripoti hiyo inaelekeza kidole cha lawama kwa vituo vya kutoa huduma za afya ya uzazi kwa kuendesha dhuluma hizo.

“Kuhusu wahudumu wa afya wanaowadhuluma akina mama, asilimia 51 kati yao ni wauguzi, asilimia 25 ni madaktari na wataalamu wa afya ya uzazi na asilimia 19 ni wafanyakazi wa vituo vya afya wasio wataalamu kama vile makarani, wadumishaji usafi, wapishi na wengineo,” inasema ripoti hiyo.

Hii ndio maana asilimia tisa ya visa vya dhuluma dhidi ya akina mama huchangia vifo vya watoto wachanga.

Aidha, asilimia 13 ya visa hivyo vina madhara ya muda mrefu kwa afya ya watoto na ukuaji wao.

Kulingana na watafiti, kati ya wanawake 25 katika kundi la waliohojiwa, watatu waliripoti kuwa walipoteza watoto wao ilhali wawili walisema kuwa watoto wao sasa wamepata ulemavu kutokana na dhuluma walizotendewa wakati wa kujifungua.

“Tangu wakati huo, matibabu waliyonipa hayakuniridhisha. Tangu wakati huo sijapata hedhi hata baada ya kutembelea hospitali mbali kutaka kujua tatizo ambalo lilinikumba,” mmoja wa wanawake Kenya walioshiriki katika utafiti huo aliambia Taifa Dijitali.

Matokeo hayo yalionyesha kuwa visa vya wanawake kupuuzwa na wahudumu wa afya, kunyimwa huduma, uchafu wa vyumba vya kujifungulia na visa vya wanawake kupewa dawa zisizo sahihi ni miongoni mwa vile vinavyoathiri wanawake.

Kwa ujumla, asilimia 83 ya wanawake 183 walioshiriki katika utafiti huo waliwahi kupitia aina mbalimbali za dhuluma katika vituo vya afya wakati wa kujifungua.

Asilimia 11 kati ya wanawake hao walikuwa ni wale wanaoishi na ulemavu.

“Kauli na majibu yalikusanywa kutoka kwa kaunti 27 katika mikoa saba ya zamani ya Nairobi, Magharibi, Kati mwa Kenya, Nyanza, Pwani, Bonde la Ufa na Mashariki,” ripoti hiyo inasema.