Maoni

Mbolea feki NCPB ni ithibati tosha walaghai wameteka nyara Kenya

April 11th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

Na LEONARD ONYANGO

TANGU kuzuka kwa sakata ya uwepo we mbolea feki katika maghala ya Bodi ya Mazao na Nafaka (NCPB), viongozi wakuu serikalini wamekuwa wakitoa kauli za kujikanganya – hali inayoibua maswali zaidi.

Kwanza, Waziri wa Kilimo Mithika Linturi alipuuzilia mbali madai hayo akisema ni porojo zilizofadhiliwa na upinzani.

Mapema wiki hii, Bw Linturi alibadili kauli na kudai kuwa mbolea duni ni magunia 3,000 pekee.

Naibu Rais Rigathi Gachagua anadai mbolea feki ni magunia 50,000 huku waziri wa Huduma ya Umma Moses Kuria akishikilia kuwa ni magunia 2,000 tu.

Rais William Ruto amesalia kimya licha ya ukweli kwamba, uwepo wa mbolea feki nchini ni pigo kubwa kwa juhudi za serikali kutaka kuhakikisha Kenya inazalisha chakula cha kutosheleza na kukomesha njaa ambayo imekuwa ikihangaisha mamilioni ya Wakenya kila mwaka.

Ufichuzi kwamba mbolea feki inauzwa kupitia maghala ya NCPB ulitolewa na mwanahabari Allan Namu kupitia runinga ya NTV. Kwa mujibu wa Bw Namu, mbolea hiyo feki iliyosheheni mchanga, inauzwa na wanasiasa ambao wanavuna mabilioni ya fedha huku wakulima wakiambulia patupu.

Baadhi ya wanasiasa wamejitokeza kumshambulia Bw Namu – ithibati tosha kwamba, madai yake kwamba mbolea feki inasambazwa na mabwanyenye serikalini yana mashiko.

Kujikanganya kwa vigogo serikalini kuhusu mbolea hiyo pia kunazua maswali tele.

Ikiwa wafanyabiashara walaghai wanaweza kuingiza mchanga katika maghala ya serikali wakidai ni mbolea, ni nini kinawazuia kujaza bidhaa ghushi madukani? Ni rahisi mno kuuzia Wakenya bidhaa ghushi madukani kuliko kuuza mchanga katika maghala ya NCPB.

Wakenya wanafaa kuwa na wasiwasi kuhusu bidhaa wanazotumia kwani ubora wazo haujulikani.

Ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa Kenya ni miongoni mwa nchi 30 duniani ambapo biashara ya bidhaa feki imenoga.

Ikiwa jirani ya nchi zinazokumbwa na machafuko ya mara kwa mara kama vile Somalia, Sudan Kusini na hata Bahari Hindi, Kenya inakuwa nafasi nzuri kwa wafanyabiashara walaghai kuingiza bidhaa feki nchini.

Hali inakuwa mbaya zaidi biashara ya bidhaa bandia inapoingiliwa na vigogo serikalini kwani hawawezi kukamatwa na polisi.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Kupambana na Bidhaa Feki nchini (ACA), bidhaa moja kati ya tano zinazouzwa nchini Kenya ni bandia – hali inayotia maisha ya Wakenya hatarini.

[email protected]