Habari za Kaunti

Mama afa akijaribu kuokoa mwanawe kwenye nyumba iliyoshika moto

April 11th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA JURGEN NAMBEKA

MWANAMKE katika eneo la Madzindani, Kaunti ya Kilifi na mwanawe mwenye umri wa miaka miwili walifariki katika mkasa wa moto uliotokea Jumatano jioni.

Bi Huldah Mahikizo, ambaye ni mhudumu wa afya katika hospitali ya Port Reitz iliyoko Kaunti ya Mombasa, alifariki alipokuwa ameingia kwenye nyumba yao iliyoshika moto ili kumwokoa mwanawe.

Mapema wiki hii, Bi Mahikizo alikuwa miongoni mwa wahudumu wa afya walioshiriki maandamano ya mgomo wa madaktari jijini Nairobi.

Kulingana na wakazi walioshuhudia kisa hicho ambao walizungumza na Taifa Leo, alikuwa katika duka lake la dawa wakati moto ulipozuka.

“Tulikuwa tumeketi chini ya mti tulipoona moshi. Tulipiga mayowe na kuita majirani. Bi Mahikizo ambaye alikuwa katika duka hilo ambalo liko mita chache kutoka kwa nyumba yake alikimbia na kurudi nyumbani kwenda kumwokoa mwanawe aliyekuwa akilala. Licha ya juhudi zake moto ulimzidi nguvu,” akasema mmoja wa majirani, Bi Agnes Kanzao, ambaye pia alishuhudia tukio hilo.

Moto huo uliteketeza chumba chake cha kulala ambako mtoto huyo alikuwa amelala, pamoja na mali ya thamani isiyojulikana iliyokuwa ndani ya chumba hicho.

Mumewe, Bw George Sewaali, alikuwa nyumbani kwa jirani mmoja wakati ambapo tukio lilitokea na alipofika kwenye tukio hakukuwa na lolote la kufanya.

“Wajenzi waliokuwa wakifanya kazi karibu pamoja na wanakijiji ndio walitusaidia. Mwanagu alikuwa amelala kama kawaida. Niliporudi nyumbani nilijaribu kumuita mke wangu ila hakukuwa na jibu lolote. Maafisa wa kukabiliana na moto walipokuja ndio tuliweza kuwafikia ila tulikuwa tumechelewa. Wote walikuwa wameshaaga dunia,” akasema Bw Sewaali.

Akitiririkwa na machozi

Akitiririkwa na machozi, Bw Sewaali alileleza kuwa alikuwa akijaribu kujitia nguvu, kwa kuwa alikuwa ameondoka na kuacha jamaa zake wakiwa sawa. Aliporudi alipatwa na mshtuko baada ya kupokea habari hizo za kutamausha. Mwanawe mkubwa ambaye yuko katika gredi ya tatu hakuwa nyumbani moto ulipozuka.

Kwa mujibu wa familia, kuna uwezekano kuwa Bi Mahikizo aliishiwa na hewa na kuanguka, kwani mwili wake ulipatikana katika bafu ya ndani ya chumba chao.

Katika juhudi za kutafuta mlango wa kuondoka chumbani, aliingia kwenye mlango wa choo, ambako alikutana na mauti.

Jirani mwingine, Bi Tabugoma Kalama, alisema kuwa kuchelewa kwa idara ya kaunti ya kuzima moto iliyoko Mariakani, kulifanya shughuli ya uokoaji kukumbwa na shida.

“Wanakijiji waliweka juhudi zote kuzima moto, wakitafuta maji kutoka kwa visima na hata kuvunja paa ili kufikia moto. Gari la kuzima moto lilifika baadaye kuchelewa sana. Tunaomba wawe wakiitikia wito haraka,” akasema Bi Kalama.

Wakazi walimwomboleza Bi Mahikizo kama mtu mzuri aliyewapenda watu na alikuwa tayari kusaidia yeyote aliyekuwa na hitaji. Walieleza kuwa walikuwa wamepata pigo haswa kwa duka lake la dawa ambalo lilikuwa likiwasaidia wengi.

Miili ya wawili hao ilikuwa imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Kilifi zikisubiri upasuaji.

Licha ya wakazi kueleza kuwa moto huo huenda ulisababishwa na hitilafu za nyaya za umeme, polisi wameeleza kuwa walikuwa wakifanya uchunguzi kubaini kiini cha moto huo.

Mwendazake alikuwa mwekahazina wa Muungano wa Wahudumu wa Afya (KUCO), wanachama wakimwomboleza pia.